WAJIBU WA VIJANA

 

Mtungaji:

Shaykh Hasan Saffar

 

Mfasiri:

Abu Ahmad Hussein

 

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

 

Jaribio la Kumfahamu

 

Kabla ya kufikia umri wa miaka kumi na mitano kwa kipindi kidogo, mwanadamu huka­biliana na kipindi muhimu na cha hatari katika uhai wake, nacho ni kipindi cha ujana (ubaro­baro) ambacho huendelea nacho hadi kufikia umri wa miaka ishirini au ishirini na tano hivi.

 

Hiki ndicho kipindi cha ubarobaro (usha­babi), nacho ni kipindi muhimu na cha hatari. Hebu tujiulize kwa nini kuwa ni muhimu na hatari?

 

Ni muhimu kwa kuwa huihukumu hali ya baadaye ya umma na mwisho wake. Vijana hawa wanaokua hivi leo bila shaka wao ndio umma wa kesho.

 

Umma huu ulioko hivi sasa utaondoka na pahali pao na vyeo vyao vitachukuliwa na hawa vijana. Naam, utawaachia pahali pake umma unaokuja, umma mpya. Nao huo umma mpya ni hawa vijana wa leo na mabarobaro wa sasa.

 

Kwa hakika ni kweli kabisa kwamba mwana­chuoni wa leo wa kidini hatakuwa ndiye mwana­chuoni wa kesho, bali hapana shaka yoyote kwamba pahali pake na cheo chake ataviacha kisha atakuja mtu mwingine miongoni mwa hawa vijana mabarobaro iIi achukue pahali pake.

 

Mkuu wa mkoa au wilaya wa leo hatakuwa ndiye mkuu wa mkoa au wilaya wa siku zijazo, bali hapana budi nafasi yake itafikia kikomo, atakufa na pahali pake patachukuliwa na mtu mwingine.

 

Vivyo hivyo, rais wa nchi wa leo, hakimu, amiri, waziri, kiongozi,  n.k. watakufa na pahali pao patachukuliwa na vilana wa leo.

 

Hii ndiyo tabia ya uhai na tabia ya maumbile. Huu ndio mwenendo wake kwamba kizazi kimoja kinapoondoka badala yake huja kizazi kingine.

 

Je, hao watu wengine watakaochukua nafasi ya jamii ya sasa katika siku zijazo ni akina nani? Hakika wao ni hawa vijana wa leo, kwani wao ndio watakaounda jamil ya kesho.

 

Siku moja Imam Hasan bin Ali AS aliwa­kusanya watoto wake na kuwaambia: "Nyiny leo ni watu wadogo, mnatarajiwa kuwa watu wazima kwa wengine."

 

Vijana wetu wa leo ikiwa watalelewa vyema hadi wawe wema na wanyofu, tunaweza kuba­shiri kuwa umma wetu na jamii zetu bali na vizazi vyetu vijavyo vitakuwa na mustakbali mwema; lakini wasipokuwa wema au wasipo­fuata njia nyofu basi itamaanisha kuwa huenda mustakbali wao ukawa mwovu, mweusi na wenye giza.

 

Kipindi cha ushababu ni muhimu sana kwa sababu ndicho upeo wa mustakbali wa umma na mustakbali wa wananchi, na kutokana na sababu hii ndio mafundisho bayana ya dini yanatilia mkazo sana kukizangatia kipindi hiki kutokana na umuhimu wake.

 

Kwa mfano kauli ya Mtume Muhammad SAW aliposema: "Hakika nyayo za mja hazita­weza kunyanyuka katika siku ya Kiyama hadi aulizwe ameumaliza umri wake katika nila gani na ameutumia ujana wake katika nini."

 

Wakati kama huu ni wa hatari kwa kijana kwa kuwa huishi katika hali maalum inayoathirika kimwili, kifikra na kijamii.

 

Katika hali hii ya pekee anayoishi kijana katika kipindi cha ujana, inatakikana ama ajiimarishe katika mazingira yaliyo mema na maongozi yaliyo salama ili aweze kuvuka kipindi hiki akiwa ni kijana mwenye juhudi sana ambaye ataweza kuunufaisha umma kutokana na kuwepo kwake na harakati zake; au aondokee kuwa ni kijana aliyeharibika katika mazingira ya ufisadi na matokeo yake iwe ni kuibomoa nafsi yake na kuibomoa jamii yake.

 

Vipambanuzi vya Kipindi cha Ujana

 

Kipindi cha ubarobaro kinajipambanua kwa wingi wa sifa na vipawa. Sifa hizi na vipawa hivi hupatikana kwa wingi katika shakhsia ya baro­baro katika pande zote za maisha yake.

 

Upande wa Kimwili:

 

Katika kipindi cha uvulana na ubarobaro, mwili wa mwanadamu hutangaza kuwasili kwake kwenye kilele cha kukomaa na kukamilika, kwani huchukua umbile lake halisi na nguvu zake hukamilika na kimo chake humuongezea urembo wa kitabia. Qur'ani Tukufu yaelezea kuwa wakati wa uvulana ndio wakati wa nguvu.

 

Mwenyezi Mungu amesema: "Mwenyezi Mungu (ndiye) ambaye amewaumba nyinyi kutoka unyonge kisha akajaalia baada ya unyonge nguvu, kisha akajaalia baada ya nguvu unyonge na uzee, Mwenyezi Mungu huumba anachokitaka na Yeye ndiye Mjuzi na Mwenye uwezo." (30:54)

 

Mwanadamu huja kwenye uhai akiwa yu mtoto mdogo dhaifu, hawezi hata kumwondoa nzi aliyetua usoni mwake, kisha hukipita kipindi hicho cha udhaifu (utoto) huenda katika kipindi cha uvulana, kipindi chenye nguvu na nishati; kisha unyonge humjia tena na kumtawala mara nyingine kwa jinsi ambayo huingia katika zama za uzee na ukongwe.

 

Vilevile katika wakati wa ujana, hisia za mwanadamu hulipuka na hisia za jinsia hazimpi nafasi. Kijana huishi katika hali ya zahama, dhiki na vurugu za kijinsia (shahawa) na huende­lea katika hali hii. Hisia hizi huwa zinahitaji kushibishwa na kuondoshewa kiu yake.

 

Upande wa Kijamii:

 

Baada ya kukipita kipindi cha utoto alipo­kuwa mdogo akinyenyekea amri za wakubwa, akiwa hana rai wala hamiliki jambo lolote, sasa huona kuwa ni barobaro. Nafsini mwake anaji­hisi kuwa ana nguvu, na kifuani mwake amejawa na hisia ya kujamini dhati yake. Wakati huo hutafuta jukumu Ia kutekeleza katika jamii.

 

Sasa yeye si mtoto tena, bali hujihisi kuwa ni mtu mzima (mme) aliyekamilika uume (utu), na ni wajibu wake kufanya yale yanayofanywa na wakubwa.

 

Umekwisha ule wakati aliokuwa akitendewa kama mtoto mdogo, wakati alipokuwa akitii amri za wakubwa na kunyenyekea matakwa yao. Hivi sasa yeye amekuwa mkubwa si mdogo tena. Anayo rai anataka aitekeleze na anatafuta jukumu katika jamii alitekeleze ili aijaze hi faragha ya kinafsi aliyokuwa nayo muda mrefu.

 

Upande wa Kinafsi:

 

Katika kipindi hiki cha ubarobaro, ndani mwa nafsi ya ubarobaro huwemo matakwa ya kutaka kukataa kila jambo na roho ya kutaka kuasi, kama kulipizia kisasi kwa aliyofanyiwa alipokuwa  mdogo, wakati alipokuwa akitii matakwa ya wazazi wake na vilevile kuzinye­nyekea ada za jamii yake bila ya kuweza kupinga au kuhalifu na kujitenga.

 

Kijana anapokuwa mkubwa na mwenye nguvu hupendelea naye atekeleze haki yake katika kupinga au kukubali na kuwa na rai huru. Huu ndio wakati ambao hukua nafsini mwake roho ya kutaka kupinga na kuasi.

 

Tena hapa kuna sifa nyingine anayosifiwa barobaro kuwa nayo katika wakati huu wa uvulana na ujana, nayo ni ule upendo wake wa kujitolea na kuwa tayari kwake kujitoa mhanga.

 

Tabia ya binadamu na umbile lake kila anapoishi muda mrefu hapa duniani, tamaa na pupa lake Ia kutaka kubakia zaidi hapa duniani huzidi kuambatana naye.

 

Ama tunapomzingatia barobaro kwa kuwa ni chipukizi anayeanza kukua katika hii dunia, yeye hawi mwingi wa tamaa na pupa Ia kutaka kubakia hapa duniani kama anavyokuwa mzee mwenye umri mkubwa.

 

Mwenye kuyachunguza kwa makini matendo ya barobaro atagundua kuwa ana tabia ya kuji­ingiza kwenye hatari au kushikilia lilelile analo­litaka, kupambana bila ya kujali kufa hasa anapo­jawa na hamasa. Ama mtu mkubwa wa umri, yeye hujihifadhi, tena huwa mwenye utulivu na husara katika matendo yake na shughuli zake. Kule kuwa kwake na majaribio humpa aina fulani ya kuwa na mizani na kujihifadhi, tena pupa lake Ia kubakia duniani halimkubalii kuwa na upendo wa kujiigiza katika mambo bila ya kuzingatia.

 

Hapa kuna mfano mwepesi kuhusu hakika hii. Hebu mpeleleze barobaro anapoendesha gari, kisha mpeleleze mtu wa makamo uendeshaji wake uko namna gani.

 

Imerekodiwa kwamba katika zama za khallfa wa Kiabbasi Harun Rashid, aliambiwa kuwa yuko mtu aliyeishi na Mtume Mtukufu na aka­sikia hadithi zake. Yeye ni sahaba aliyekuwa na umri mrefu ambaye aliishi tokea zama za Mtume Mtukufu hadi zama za Harun Rashid. Umri wake ulikaribia miaka mia moja na thelathini (130)

 

Kwa vile sahaba huyu ana heshima kuu, Harun Rashid alipendelea kukutana naye. Harun Rashid akaamuru aletwe na akaletwa kwake huku amebebwa. Harun Rashid akamwuliza:

"Je, wewe umekutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

Mzee  akainamisha kichwa chake  kama kuonyesha alama ya kujibu ndio.

 

“Je,  umewahi  kuyasikia  mazungumzo (hadithi) ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

 

"Ndio.”

 

"Je,  unakumbuka mazungumzo yoyote miongoni mwa mazungumzo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu?"

 

"Ndio”

 

"Hebu nizungumzie iIe hadithi unayoikumbuka uliyoipokea kwa Mtume Mtukufu."

Mzee akasema kwa sauti dhaifu sana: "Nime­msikia Mtume wa Mwenyezi Mungu siku moja akisema: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili -tamaa na matumaini.”

 

Mzee akayakata mazungumzo huku akiwa hana uwezo wa kuendelea nayo.

 

Harun Rashid akaamuru apewe zawadi, nayo ilikuwa ni kiwango fulani cha mali, na iliwekwa juu ya kitanda chake. Kisha wakambeba ili kumrudisha nyumbani kwake.

 

Harun Rashid akahisi kwamba mdomo wa sahaba mzee  ulikuwa ukichezacheza kana kwamba alikuwa akisema kitu.  Akaamuru arejeshwe. Watumishi wakaja naye hadi ubavuni karibu na Harun Rashid. Akamwuliza: "Nimeiona mdomo wako ukichezacheza wakati ulipokuwa ukirudishwa kana kwamba ulikuwa ukisema kitu."

 

Mzee akasema: "Ndio, nilikuwa nikiwauliza waliokuwa wakinibeba: 'Je, huyu Harun Rashid ataifanya zawadi hii iwe ni ya kila mwaka, awe akinipa mfano wake ili niweze kumzuru mwanzo wa kila mwaka?'”

 

Harun Rashid akacheka, kisha akasema: "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema kweli kabisa katika ile hadithi uliyolsema hivi sasa kwamba: 'Mwanadamu huzeeka na hubakia ndani mwake sifa mbili - tamaa na matumaini.’”

 

Hivi ndivyo ilivyo. Tamaa ya mwanadamu na matumaini yake ya kutaka kuishi duniani huzidi kukua nafsini mwake kila umri wake unapozidi. Hubakia ana busara na hujihifadhi katika matendo yake na mambo yake yote, ambapo barobaro huwa yuko tayari kujitoa sadaka na kujiingiza katika mambo ya hatari bila ya kujali hatari zilizoko mbele yake.

 

Upande wa Kifikra:

 

Aghlabu vijana na barobaro katika kipindi hiki cha ujana huwa na faragha na udhaifu wa kiakili katika kufungamana kwao na watu.

 

Katika kipindi hiki cha ubarobaro akili ya binadamu hufumka na vipawa vyake hufunguka. Huanza kuyafikiria mambo kwa undani. Akilini mwake huchoreka maswali mengi kuhusu maisha yake na maisha ya jamii. Maswali ambayo hayana budi kujibiwa wazi.

 

Vilevile hujiona kwamba halazimiki tena kuzikubali fikra za watu wake na mazingira yao, madamu ameamini nafsini mwake kuiamini dhati yake, na kupendelea kufuata mtindo wa kukataa na kupinga kila jambo na kupondokea zaldi upande wa kubeba majukumu mazito mazito na ya hatari.

 

Kwa ajili hiyo, barobaro huwa yuko tayari kuipokea na kuifuata fikra yoyote mpya japo iwe ya hatari namna gani.

 

Ama mtu mkubwa yeye ana ukinaifu, imani na fikra anazoziamini na kuzitukuza miaka mingi. Yeye hana faragha ya kiakili wala hahisi kuwa na haja ya kuwa na itikadi nyingine mpya, bali yeye hayuko tayari kuiacha fikra aliyoiamini muda mrefu na kuitukuza miaka mingi.

 

Kwa ajili hiyo utaona kwamba kila ujumbe na mafunzo kutoka mbinguni yalisimama na kupata nguvu kutokana na mabarobaro (vijana) wale ambao kwamba wao huwa wepesi kuziamini hizo fikra mpya na huwa tayari kujitoa mhanga kwa ajili ya kuzitetea.

 

Tuchukue mfano mmoja: Nabi Ibrahim AS alipowapelekea watu wake ujumbe wa kumpwe­kesha na kutomshirikisha Mwenyezi Mungu, ni nani aliyemwamini na kuukubali wito wake? Watu wake hawakuukubali ujumbe wake, isitoshe wakamtuhumu kwa kuwa aliaminiwa na kikundi cha vijana maskini, kama Qur'ani Tukufu inavyosema: "Na hatukuoni wamekufuata isipo­kuwa wale wanyonge katika sisi wenye fikra ya mwanzo." (11:27)

 

Naye Nabii wetu Muhammad SAW pia. Wale waliofanya upesi  kumwamini na kuufuata ujumbe wake walikuwa ni kikundi cha mabaro­baro, wadogo kwa umri, kama Ali bin Abu Talib AS, Bilal Mhabeshi na Ammar bin Yaasir, n.k.

 

Jambo hili liliwafanya wazee na viongozi wa Makureshi kumtuhumu Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amewaharibu vijana wao na wakayasema hayo hayo katika mashitaka yao waliyoyapeleka kwa ami yake, Abu Talib. Waka­sema: "Hakika mwana wa nduguyo amewatusi miungu wetu, na amezipuuza ndoto zetu na amewaharibu mabarobaro wetu."

 

lli kuitilia nguvu hakika hii, Mtume Mtukufu amesema: "Nawausia kuwafanyia mabarobaro wema, kwani wao wana mioyo laini zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amenituma mimi  (niwe) mbashiri na mhofishaji, mabarobaro wakaapa kushikamana nami na wazee wakanihalifu... Na muda wao (wa kuishi duniani) ukawa mrefu na nyoyo zao zikasusuwaa (zikawa ngumu)."

 

Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib ame­sema: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa) chochote kinacho­ingizwa (kinacholimwa) ndani yake hukikubali."

 

Vipi Tufaidike katika Kipindi cha Ubarobaro

 

Hayo yote yaliyotangulia ndiyo mambo muhimu na sifa muhimu zinazompambanua barobaro zikiwemo sifa za machimbuko yaliyo hatari pia.

 

Kwa hivyo, imetubainikia kwamba ni kwa miongozo mema na taratibu zilizo salama tu, ndipo itamkinika kufaidika na hivi vipawa na kuvipatiliza katika kuujenga utu wa Kiislamu unaotakikana ili vijana wetu wawe ni mfano halisi wenye kufanana na maisha ya vijana wa Kiislamu waliopigana jihadi kama Ammar bin Yaasir, Mus'ab bin Umayr, Malik Ashtar na Al bin Husayn al-Akbar.

 

Ikiwa tutawapuuza vijana wetu na kutowajali katika wakati huu ulio hatari au tukawatendea vibaya katika sifa zao na vipawa vyao vya kifikra, huenda tukaonjwa kwa kupata umma mpya uliopotoka na kuharibika. Umma huu mpya utapotosha njia na lengo, na vilevile utaubomoa mustakbali wake mwema.

 

Swali Ietu hivi sasa ni hili: Ni kwa njia gani tutafaidika  na  wakati  huu  wa  ubarobaro (uvulana)? Vipi tutavikuza vipawa vyake na kumpangia nyadhifa kwa ajili ya maslahi yake na kuujenga utu wake, ili aweze kuubeba wajibu wa ujumbe huu wa Kiislamu? Haya ni miongoni mwa yale yatakayomfanya kijana awe ni msingi mwema wenye utendaji katika maendeleo ya kijamii na kuuendeleza mbele ujumbe huu wa Kiislamu.

 

Hapa napendelea kuelezea kwa kirefu kila kipawa cha kipindi hiki cha uvulana, na kuya­elezea mambo yenye kumpangia wadhifa na kumwongoza kwa ajili ya kujenga viongozi miongoni mwa vijana na umma wa Kiislamu unaokuja. Hapo tutaona vipi tutaweza kufaidika na kila kipawa chake, miongoni mwa hizi sifa tulizozitaja wakati atalelewa na kukua katika maongozi sahihi.

 

Vikwazo vya Matamanio ni

Fursa Nzuri ya Kuimarisha Matakwa

 

Ikiwa vijana wa umma wanamiliki irada (matakwa) na nguvu ya nafsi iliyo thabiti ambayo inashinda matamanio ya nafsi, nia na Irada thabiti yenye kupambana na ghururi, hakika umma utakuwa umetukuka na kupata heshima kuu. Tena umma kama huu utakuwa una uwezo wa kukabiliana na maadui na kupambana na wakoloni. Hautaweza kurukuu na kuyaitikia matakwa ya wakoloni, na hautamnyenyekea dhalimu  au  kuridhia kuwa  watumwa  wa wadhalimu na wakoloni.

 

Umma ni muundo wa mkusanyiko wa watu. Ikiwa watu wanaounda umma ni watu walio­pondokea kwenye uharibifu na maovu, na ni wenye tabia ya ghururi na shahawa, basi msimamo wa umma na muamala wao kwa maadui zao utakuwa ni baridi na wenye kuku­baliana na maovu hayo na dhuluma hiyo.

 

Ama ikiwa watu wanamiliki irada (nia thabiti), nguvu ya nafsi na uwezo wa kupambana na vikwazo, hakika umma ukishikana na vijana wake unaweza kukabiliana, kupinga na kusimama kwa ushujaa dhidi ya tamaa za maadui na njama za madhalimu na wakoloni.

 

Wakati huu wa uvulana ni fursa nzuri yenye thamani ya kuikuza irada (matakwa) ya mtu katika umma. Sababu ni kwamba irada ya bina­damu haipati nguvu mara moja kwa kuipa mawaidha au kuipa miongozo, bali hupata nguvu kwa kupitia ukinzani na kwa kupambana na ghururi na vikwazo vya kila aina.

 

Kwa mfano, mtu ambaye ataikuta nafsi yake imezingirwa na mambo yenye udanganyifu na hadaa zenye nguvu, tena ikawa nafsi imebanwa katika vikwazo vyenye shahawa kali, yamkinika kwake kuilelea nafsi yake kwa matendo, kwa kuwa mgumu wa kutoyatii matamanio yake, aikuze kwa kuiviza irada yake kwa majaribio ya kimatendo. Mtu kama huyu anaweza kupata ushindi, hasa pale atakapoitukuza nafsi yake na kuzidharau zile ghururi na shahawa na aikanye nafsi  yake  kuvinyenyekea  vikwazo  vya matamanio.

 

Vivyo hivyo, kipindi hiki cha ujana kwa vijana ni kipindi cha kuipa mazoezi irada na kuifanyia majaribio nafsi yake.

 

Kijana akipata miongozo iliyo salama na kupata mafunzo (elimu) sahihi yaliyojaa ubina­damu katika malezi yaliyo mema, ataweza kuya­pita majaribio haya kwa ushindi mkubwa, na baada ya mtihani huu atakuwa mwenye irada yenye nguvu na ushujaa.

 

Hakika mara nyingi mabarobaro husumbu­liwa na hisia kali za matamanio nafsini mwao, vilevile hupambana na ghururi (hadazi) za aina mbalimbali zenye nguvu, lakini huweza kupata ushindi upesi hasa anapoweza kuitawala nafsi yake, kuuhifadhi utu wake na heshima yake, akaweza kupambana na hadazi zote na akaweza kujiepusha na vitimbi vikubwa vya matamanio yenye kiwi, hasa katika hizi jamii zetu kunako­patikana kwa wingi upondokeaji kwenye uhari­bifu na ufisadi. Barobaro akiweza kuyashinda hayo yote, yamaanisha kwamba ameimiliki irada yake iliyo thabiti na amemiliki nafsi yenye kutoteteleka. Wakati ambapo umma utamiliki watu pamoja na vijana wa namna hi basi hapo utaweza kuwa na matumaini ya kuwa na mustakbali mwema.

 

Riwaya na hadithi tukufu zilizopokewa katika mafunzo matukufu ya Qur'ani zimeelezea kwamba barobaro anayo sifa tukufu ya kuyapa nyongo mambo yenye ghururi na ya haramu kwa kutubu, kwani toba inadhihirisha kuji­hifadhi kwake na kulingana kwake. Mtume Mtukufu amesema: "Toba ni nzuri, na kwa barobaro ni nzuri zaidi."

 

Pia  imepokewa  kwake kuwa amesema: "Hakuna kitu kizuri kinachopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kumwona barobaro mwenye kutubu."

 

Ni kwa nini kitendo hiki kinamfurahisha Mwenyezi Mungu? Sababu ni kwamba barobaro anapojiondoa kwenye maasi na kuyadhibiti matamanio yake huwa amefanya ukinzani mkubwa dhidi ya nafsi yake, vilevile huwa anailelea nafsi yake juu ya misingi ya kupania, kukakamia na kushikamana na imani yake.

 

Tunapoidurusu historia ya viongozi wakubwa wa historia ya binadamu, tunakuta kwamba aghlabu yao walikuwa na jitihada ya hali ya juu sana wakati wa ujana wao katika kuzijenga nafsi zao na kuzielekeza kwenye maongozi matukufu yenye utu na ukamilifu. Na sababu ni kwamba wao walishikamana na mkondo wa matukufu na kulazimiana nayo, na wakakataa kupomoka kwenye lindi Ia matamanio na upotevu wenye kutenganisha na haki, pamoja na kwamba kuli­kuweko hali zenye kusaidia kuwavuta kwenye matamanio na kuzama zaidi kwenye mambo ya ufisadi.

 

Hebu tujionee baadhi ya kumbukumbu za maisha ya baadhi ya viongozi wakuu ambao wamefaidika kwa kuziviza irada zao katika wakati wa ujana wao, wakazipa nguvu nafsi zao kwa kukakamia kujiepusha na shahawa za nafsi. Kutokana na kufuata njia hii, walizipa nafsi zao nafasi ya kwanza ya kuyavaa matukufu na kuvi­kwea vilele vya matukufu na ukamilifu.

 

1.                  Hebu tuitazame historia ya Nabii wa Mwenyezi Mungu, Yusuf bin Yaakub AS akiwa ameyakosa malezi ya wazazi wake pamoja na huruma yao tokea udogoni mwake baada ya kumpoteza mama yake, ndugu zake walimlia njama na kumtupa kisimani, kisha akanunuliwa na mmoja wa misafara ya Misri kwa thamani ya chini ya dirhamu chache.

 

Tazama ndugu msomaji, majaaliwa yalitaka aishi katika zama zake za ubarobaro ndani mwa nyumba ya Mfalme wa Misri pamoja na mkewe Zulaikha ambaye alivutwa vilivyo na uzuri wa Nabii  Yusuf  AS uliojulikana na uliokuwa ukipigiwa mfano. Ashiki ya kumpenda Yusuf ikavama moyoni mwa Zulaikha, na nyumba walimokuwa  wakiishi  haikuwa  na  yeyote mwenye kutia zahama, na hali haikuwa na pingamizi yoyote ya kuzuia kutekeleza hila za kishetani.

 

Hebu sawirisha ewe kijana uliye barobaro, kuwa wewe umeingia kwenye mtego wa Nabli Yusuf AS. Pia chukulia kuwa uko katika mazingira yanayosaidia kupotoka, Je, ungefanya nini? Na wajibu wako ungekuwa ni nini katika hali kama hii?

 

Naam, ukweli ni kwamba wengi wa barobaro wetu wa sasa, mara nyingi wanatatizwa na ghururi zilezile ambazo zilimtatiza huyu baro­baro mtukufu Yusuf, vilevile wanaishi katika mazingara sampuli ileile aliyoishi.

 

Kwa hivyo, ni juu ya vijana wetu kumfanya Nabii Yusuf AS kuwa ni kiongozi wao na kugizo chao, wamwige katika kupambana kwake na ghururi kama zile katika kukabiliana kwake na hali kama zile. Hebu tutazame msimamo wake ulikuwa namna gani?

 

Qur'ani Tukufu yatusimulia kwa ufasaha mkubwa ikitumia njia yake ya kimbinguni. Yatutolea baadhi ya visa vinavyoelezea baadhi ya ile mikasa hatari aliyoipata Nabii Yusuf AS katika nyumba ya Mfalme wa Misri, pamoja na tukio Ia kurukiwa na Zulaikha. Mwenyezi Mungu asema:

 

"Na akasema yule aliyemnunua huko Misri kumwambia mkewe: 'Mweke pahali pazuri huenda akatufaa au tukamfanya mwana. 'Na hivi ndivyo tulivyommakinisha Yusuf katika ardhi (nchi,) ili tumfundishe taawili (ufafanuzi) za hadithi na Mwenyezi Mungu ni Mshindi juu ya jambo Lake lakini watu wengi hawajui. Na alipo­fikia ukamilifu wake tukampa hukumu na elimu na vivi hivi huwalipa wonaofanya wema. Na akamtaka [Yusuf kutenda  haramu] yule [Zulaikha] ambaye yeye yuko nyumbani kwake nafsi yake, na akafunga milango [ili asikimbie] na akasema: 'Ni toyari njoo [nimejitayarisho kwa ajili yako].' Akasema [Yusuf]: 'Namwogopa Mwenyezi Mungu, Yeye ni Mlezi wangu, ameyafanya mazuri makao yangu. Hakika madhalimu hawafuzu.' " (12:21-23)

 

Qur'ani inaendelea kuyafafanua baadhi ya maelezo ya kisa chenyewe kutokana na umuhimu wake hadi pale ilipomdondoa Zulaikha akisema:

 

Hakika nilimtaka nafsi yake akajizuia (akakataa) na ikiwa hatafanya ninayomwamuru, atafungwa na atakuwa katika wanyonge.' Akasema [Yusuf]: 'Mola wangu, jela ni boro zaidi kwangu kuliko yale wonayoniita kuyafanya, na ikiwa hutaniepusha na vitimbi vyao, nita­pondokea kwao na nitakuwa miongoni mwa wajinga.' Basi Mola wake akamjibu, akamwepu­shia vitimbi vyao; hakika Yeye ni Mwenye kusikia na ni Mjuzi." (12:32-34)

 

Vivi     hivi Yusuf alimwomba Mwenyezi Mungu amsaidie katika kupambana na ghururi za matamanio na hali za upotofu. Naye Mwenyezi Mungu akayajibu maombi yake, na Nabii Yusuf akazishinda zile hali zote za uharibifu na ufisadi ingawa alistahamilia maovu na kwa muda mrefu alibaki jela kwa azma, nia thabiti na nafsi yenye ushujaa. Na hivi ndivyo inavyotakikana kijana mwema awe.

 

2.                  Kuna kisa kingine chenye kuvutia na kustaajabisha  kama  kinachoelezwa katika historia. Kisa chenyewe kinamhusu Sayyid Mir Damad, aliyekuwa mwanachuoni mashuhuri sana nchini Iran.

 

Yaelezewa kwamba Sayyid huyu alifikiwa na kisa hiki wakati akiwa kijana mbichi mwanzo wa kubalehe kwake, naye alikuwa ni mwanafunzi katika madrasa moja ya kidini katika jiji Ia Tehran. Katika usiku mmoja wakati binti wa Shah wa Iran katika zama hizo alipokuwa akitembea mitaani pamoja na vijakazi na watu­mishi wake, kwa ghafla kukanyesha mvua kubwa na kukavuma upepo mkali na kila mmoja miongoni mwa watumishi wa binti wa Shah akakimbia kutafuta mahali pa kujificha kibinafsi. Binti wa Shah akabakia peke yake mitaani katika lile janga Ienye kutisha na kuhofisha, ikawa naye hana budi kutafuta pahali pa kujificha. Katika kutazamatazama kwake huku na huko iIi angaa naye apate pahali pa kujificha na kujistiri, akauona mlango wa madrasa uko wazi, akaingia madrasani. Kwa bahati akagonga mlango wa chumba cha huyu Sayyid kijana na akamkuta yuko kando ya moto akijiota ili ajiondoshee baridi aliyokuwa nayo.

 

Binti huyu akamwelezea huyu Sayyid kijana kisa chake, kwamba yeye ni msichana aliyepotea njia na anachohitaji ni msaada, pahali pa kulala na kujistiri usiku ule, hadi hali ya anga iwe tulivu na ipambazuke.

 

Sayyid aliona hana budi kulijibu ombi lile Ia msichana,  hivyo  akamkaribisha  chumbani mwake, yeye akakaa katika kipembe kimoja na msichana naye akakaa katika kipembe kingine.

 

Baada ya kupita muda katika usiku huo, shetani akaanza kucheza mchezo wake mwovu katika hali kama hii, kama ilivyopokewa katika hadithi ikisema: "Mwanamume hakai faragha na mwanamke ila shetani anakuwa wa tatu wao."

 

Shetani akawa anamshawishi Sayyid huyo kijana namna ya kuipatiliza hii fursa na kutenda haramu kwamba mambo yote yako sawa kwa kila njia, mlango umefungwa, wala msichana hana njia yoyote na kujikinga au kujitetea.

 

Lakini vipi itakuwa? Kwani Sayyid huyo alikuwa ni kijana mwema na mwongofu, anaye­tambua hila na vitimbi vya Shetani. Akawa anafikiria njia ya kujiepusha kutokana na makucha haya ya shahawa na mtego huu wa Shetani. Mwishowe akafikia kwenye uamuzi mgumu. Akaamua kuitumia njia hii kwa ajili ya kupambana na shahawa zake na kuutatua wasi­wasi wa shetani. Uamuzi wenyewe ukawa ni kuweka kidole chake juu ya kaa Ia moto, hadi ashughulishwe na uchungu wa kuchomeka ili asifikirie mambo ya haramu. Naam, aliendelea kujichoma hivihivi usiku kucha, huku akistah­milia uchungu na maumivu na huku akiihutubia nafsi yake: "Onja moto wa dunia ili uuogope moto wa Akhera!"

 

3.                  Je, ndugu! Vijana wamewahi kukisikia kisa cha lbn Siriin ambaye alikuwa mwanachuoni mkubwa wa elimu ya nafsi na aliyejulikana kwa kufasiri ndoto?

 

Katika wakati wa ubarobaro wake Ibn Siriin alikuwa mwenye umbo jema, kiwiliwili kizuri, mwenye uso mwangavu na uzuri wa kitabia wenye kuvutia. Alikuwa akifanya kazi kwa mfanya biashara mmoja wa nguo. Siku moja alifika mwanamke dukani kununua vitambaa, alipomaliza kununua mahitaji yake, akamtaka yule mfanya biashara amtume mfanyakazi wake Ibn Siriin ili ambebee mizigo yake aliyonunua hadi nyumbani kwake, kisha ampe ujira. Ibn Siriin akabeba mizigo na kuandamana naye hadi nyumbani, walipoingia nyumbani mwanamke huyo akafunga milango, kisha akamtaka afanye naye kitendo cha haramu, lakini yeye akakataa. Mwanamke alipoona amekataliwa akazidi kutumia hila za kumlazimisha zaidi. Mwisho Ibn Siriin alijiona kuwa ametumbukia mtegoni, na hapana budi kufikiria njia ya kujisalimisha kutokana na mtego huo Alipoigundua hila yenyewe alimwomba huyo mwanamke amruhusu aende chooni kujisaidia. Mwanamke akamruhusu kufanya hivyo, naye alipoingia chooni tu aliji­paka mavi mwili mzima, kisha akamtokea mwanamke yule akiwa katika hali kama hii ya kunuka. Mwanamke alipomwona katika hali kama ile, akamkimbia na kumfukuza nyumbani. Na kutokana na hila kama hii lbn Siriin alijiokoa kutoka mtego huu wa matamanio yaliyo na ghururi.

 

Wajibu wa Vijana katika Jamii

 

Vipawa vingi vya binadamu huchimbuka katika wakati huu wa ujana. Huwa na ukunjufu wa wakati na nafsi. Vilevile huwa anamiliki nguvu, uwezo na nishati. Hivi vyote vinampa nafasi nzuri na kumshajiisha kuwa na wadhifa maalum katika jamii.

 

Hapo mbeleni tuliwahi kuelezea juu ya matakwa ya kijana yenye kiwi ya kutaka kuteke­lezwa, na kupenda kwake kushiriki katika nyadhifa mbalimbali ili ahisi kwamba yuko huru na awathibitishie wengine uwezo wake na uume wake baada ya kuwa alikuwa mdogo akiishi katika hali ya kuwanyenyekea wengine na kupondokea kwenye matakwa yao. Baada ya kuwa alikuwa akitendewa kama mtoto mdogo, sasa ataka atendewe na jamii kama mtu mkubwa, mwenye heshima yake kamili na mwenye matakwa na irada.

 

Lau twampa nafasi kijana na kumuacha kutekeleza nyadhifa na wajibu anazoziweza katika jamii, na tukamwelekeza kufanya mambo mema Yenye faida na kumsaidia kuujenga utu wake na kuvikuza vipawa vyake, hakika tuta­kuwa tumefanya wema kwa kuyajua na kuya pambanua yale yanayoweza kumdanganya katika wakati wa ubarobaro. Na ikiwa hatutashughulika na masiala haya na ikawa hatutampa nafasi barobaro kutoa maoni yake na kutekeleza matakwa yake katika nyadhifa za kijamii kupitia maongozi mema, basi natija itakuwa moja kati ya mambo mawili:

 

Ima vipawa vya barobaro vitafifia, na vita­zimika au vitakufa na matumaini yake yata­zikika, au atajiingiza katika kutekeleza mambo yaliyopotoka na kufanya mambo maovu ya ufisadi. Na huu ndio mushkili unaoutatiza umma wetu wa Kiislamu.

 

Jamli nyingi hazijajua vipi zishirikiane na vijana wao katika upande huu. Wazee wengi pamoja na viongozi wale wanaoyatawalia mambo ya wananchi na kushikilia hatamu za uongozi, aghlabu yao hawako tayari kuwapa vijana wao fursa ya kutumia ujuzi wao na vipawa vyao, hawawapi nafasi yoyote ya kusimamia jambo lolote la kijamii, na hawawaamini, bali huwa­zingatia kuwa ni watoto wasiojua kitu na walio dhaifu.

 

Kutokana na sababu hii vijana wetu hukua huku wakiwa na juhudi chache sana na maarifa yao huwa ni ya daraja Ia chini. Hivyo, hupotoka na kuiacha njia ya utukufu yenye utengevu, hasa wanapochukuliwa na makundi mengine ya upotevu na kupewa nyanja za kuziamini nafsi zao na kupewa nyadhifa za kujishughulisha na mambo muhimu yaliyo hatari.

 

Kitabia, utamwona kijana akivutika kwa urahisi na kujiingiza katika lile kundi ambalo linashughulikia vyema na kumthamini kama mtu mwenye nguvu. Na utamwona mara moja anawa­acha wale watu ambao wanaoshughulikiana naye kama mtoto mdogo au kijana dhaifu.

 

Tunasikitishwa sana kuona ya kwamba jamii yetu hadi sasa haijaacha kuwapima watu na kuwapa kima (hadhi na heshima) kupitia kipimo cha umri. Imekuwa kwamba kabla kijana haja­kata masafa marefu ya umri, basi jamii ya watu wakubwa hawamwangalii kwa jicho Ia uaminifu na heshima, wala hawampi nafasi ya kutaharaki au kuwa na nishati yoyote.

 

Mtukufu Mtume ameitangaza wazi rai ya dini ya Kiislamu na akaelezea waziwazi juu ya kukataa kwake kipimo cha umri na miaka, na akafafanua kwamba kipimo cha pekee kilicho sahihi ni kipimo cha ujuzi na matendo, na kwamba kijana mwenye ujuzi na matendo anayestahili na ni bora zaidi na anayo haki ya kutangulizwa kuliko mwingine yeyote.

 

Mtume Mtukufu alimtawalisha Ittaab bin Usaid mjini Makka, juu ya kuwa umri wake wakati huo ulikuwa ni miaka Ishirini na moja. Akamwamuru kusalisha sala ya jamaa na kusima­mia shughuli nyinginezo kwa niaba ya Mtume Mtukufu. Kijana huyo alikuwa ni amiri wa kwanza kusalisha jamaa mjini Makka baada ya kukombolewa  mji  huo.  Mtume  Mtukufu alimwambia: "Ewe Ittaab!  Unajua nimeku­tanguliza kwa watu gani? Nimekutanguliza na kukufanya mwakilishi wangu kwa watu (waja) wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na lau ningekuwa namjua aliye mbora zaidi kukushinda wewe ningemteua."

 

Baadhi ya wakaazi wa Makka walipopinga uteuzi huo, Mtume Mtukufu alisema: "Mtu asihoji kwa hoja ya udogo wa umri wake, kwani ukubwa si ubora, bali ubora ndio ukubwa."

 

(Jawaan,  Sheikh  Muhammad  Taqi  Falsafi; uk. 30).

 

Vilevile taaluma za Kiislamu zinashajiisha kuvikunjulia vipawa hivi vya vijana chipu­kizl ili vivie na kuendelea. Kwa mfano, utaona katika vitabu vya fiqihi kuna masiala ambayo yanaruhusu vijana wasiobalighi bado kuwa­ongoza vijana wenzao katika sala ya jamaa; na hii ni kwa sababu ya kumpa kijana moyo na kumshajiisha ili akulie na hisia ya kuiamini nafsi yake, kwani vijana wanapoona kuwa wana sala yao ya jamaa, watatambua kwamba wame­thaminiwa na kwamba wao pia wanaweza kuwa viongozi kama walivyo watu wazima.

 

Wakati tunaposoma sera za viongozi wa Kiislamu na historia ya maisha yao, tunaona wazi kwamba wao wanaamiliana na vijana muamala wa kuwashajiisha na kuwaheshimu. Vilevile huwapa heshima kubwa wale vijana walio na ujuzi, na mara nyingine huwatwisha majukumu mazito zaidi na ya hatari.

 

Angalia jinsi Mtume wetu Muhammad SAW alivyomchagua Musa'b bin Umair, yule kijana mwenye imani na mpiganaji jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, awe balozi wake mjini Madina, ili auongoze umma wa huko katika njia ya Uislamu, autayarishe mji wa Yathrib kuwa makao ya machimbuko ya Uislamu na makao makuu ya serikali yake changa.

 

Mus'ab alifika mjini Madina akiikuta katika hali nzito kutokana na tofauti iliyokuwepo baina ya makabila ya Aws na Khazraj. Akiwa amebeba ule wajibu mkubwa kuiongoza Madina, Mwenyezi Mungu amemwafikia kufaulu katika kutekeleza wajibu huo kutokana na imani yake ya kweli, ikhlasi aliyovama moyoni na jihadi yake thabiti.

 

Katika  tukio  jingine  lenye  kuthibitisha hakika kama hii katika uhai wake wa mwisho, Mtume Mtukufu aliandaa jeshi kubwa Ia kupi­gana na Warumi mkiwemo ndani mwake masa­haba wakubwa na wazee wa Kiislamu. Uongozi wa jeshi hilo katika vita hivyo alipewa Usama bin Zaid ambaye alikuwa ni kijana asiyefikia hata umri wa miaka ishirini. Na wengine walio­kuwemo katika jeshi hilo lenye kunyenyekea uongozi na amri za Usama walikuwa ni Abubakr, Umar na Abu Ubaida ibn Jarraah, Abdul Rahman bin Auf, Talha, Zubair, n.k.

 

Baadhi ya masahaba waliudhika kutokana na uamuzi huo wa Mtume Mtukufu wa kumtangu­liza Usama bin Zaid juu yao kutokana na umri wake mdogo, habari hiyo ikamfikia Mtume Mtukufu, naye akaghadhibishwa sana na kitendo hicho cha kumthamini mtu kulingana na kipimo cha umri ambacho kilikuwa kikitumiwa wakati wa Ujahilia. Kitendo hicho kilimfanya Mtume Mtukufu kutoka na kwenda msikitini kuwa­hutubia watu, juu ya kuwa na shida ya maradhi aliyokuwa nayo na kuumwa kwake.

 

Miongoni mwa yale aliyoyasema katika hotuba yake siku hiyo ni: "Enyi watu! Ni nini haya maneno yaliyonifikia yaliyosemwa na baadhi yenu kwa sababu ya kumtanguliza kwangu Usama? Ikiwa mwapinga kumtanguliza kwangu Usama, hakika mlitangulia kuupinga (uamuzi wangu wa) kumtanguliza baba yake hapo mbeleni. Naapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba baba yake alikuwa anastahiki uongozi, na hakika mwanawe baada yake naye anastahiki uongozi pia." (an-Nass wal ljtihad, uk. 9).

 

Naye Imam Jaafar Sadiq AS alimkuta kijana Hisham bin Hakam kuwa na vipawa vikubwa na akawa akimdhihirishia mapenzi na heshima yake juu yake kwa kiasi kikubwa mpaka wazee waka­ingiwa na wivu mioyoni mwao.

 

Katika kitabu cha Safinatul Bihar imeelezwa kwamba heshima na cheo cha Hisham bin Hakam vimefikilia daraja Ia juu kabisa mbele ya Abu Abdillah Jaafar bin Muhammad Sadiq AS na kwamba Hisham alifika kwa Imam katika Mina, wakati alipokuwa anaanza kubalehe. Katika kikao hicho cha Imam walikuwepo baadhi ya masahaba zake wazee kama Hamraan bin Aayun, Qais al-Maasir, Yunus bin Ya'kub, Abi Jaafar al-Ahwal na wengineo, na Imam akampa Hisham heshima kubwa kushinda wazee wote walio­kuwepo hapo.

 

Abu Abdillah alipoona kwamba kitendo hicho kilikuwa kikubwa mbele ya masahaba wake, alisema: "Kijana huyu ametunusuru kwa ulimi wake, moyo wake na mikono yake." (jz. 2, uk. 719)

 

Kauli ya mwisho juu ya maelezo haya yataki­kana ifahamike kwamba haiwezikani kabisa kumwacha au kumtenga barobaro huku tukivi­puuza vipawa vyake. Haimkiniki kumtupa na kumwacha abakie akiwa hana thamani yoyote au atenganishwe na maisha ya umma. Hakika yatakikana athaminiwe na aheshimiwe na apewe wajibu muhimu azitekeleze na vilevile aongozwe iIi aujenge utu wake. Bila shaka, ikiwa sisi tutamshajiisha na kumpa miongozo yenye kufaa, tutafaidika naye; na hayo yatakuwa ni mataya­risho muhimu ambayo yatamjenga na kumfanya awe chimbuko jema lililo muhimu katika siku zijazo. Na ikiwa tutampuuza na kudharau rai zake na uwezo Wake na hatutompa nafasi ya kushughulika na jambo lolote au kumshajiisha na kumtia nishati na kumwongoza katika njia sahihi, tujuwe wazi kwamba atatekwa na wengine na kufaidiwa na wengine, na watamtayarisha kulingana na taratibu zao na miongozi yao miovu yenye kupoteza na kupotosha.

 

Majaribio  mengi  yamethibitisha kwamba kijana anapopewa nyadhifa au shughuli za kijamii kuziendesha au kusimamia wajibu wa kidini, huwa yuko tayari kutoa juhudi zake zote kuushughulikia umma wake, tena hushikamana zaidi na kulazimiana zaidi na dini.

 

Ama kule  kuwahimiza vijana kusali na kufunga na kuwahimiza kusikiliza hotuba na mihadhara pekee hakutoshelezi hata kidogo kudhamini utengevu wa vijana hao wala uongofu wao, wala hakutoshelezi kuyalelea maadili yao na vipawa vyao. Ni wajibu ulioko juu yetu kuwapa nidhamu na mipango yenye kuwa­taharakisha na kuwapa nishati. Nidhamu hizo ziwe nzuri ili ziweze kuwatambulisha umuhimu wao katika jamii.

 

Miongoni mwa mambo yanayotia uchungu moyoni ni upinzani unaotoka kwa jamii kuwa­pinga vijana waumini, au kikundi chema kilicho­jitolea kusimamia na kutekeleza nishati muhimu za kijamii au za kidini.

 

Umma huwawekea tuhuma na shaka na huwapinga. Mara ngapi tunayashuhudia makundi ya vijana wema wenye nia safi kwa umma wao, vijana walio na hamasa kwa ddini yao, wanaotaka kusimamia jambo la kidini au la kijamii, au kuunda kamati za maendeleo ya kidini na kijamii, lakini kwa masikitiko utaona jamii hufanya ubahili katika kuwashajiisha na kuwatia moyo. Utaona  hawawashajiishi  hata  kidogo,  bali huzuia misaada yao katika pande zote na mara nyingine huwapinga na huwawekea vikwazo. Kwa nini? Je, ni kwa kuwa baba zetu na viongozi wa jamii hawajui tabia ya kipindi hiki cha ujana, wala hawajatambua hatari yake? Au ni kwa kuwa hao wazazi na viongozi hawataki kuwa­ruhusu vijana washirikiane nao katika kuya­ongoza mambo ya kijamii kwa lengo la kuiende­leza hadhi yake? Basi ni kwa sababu gani? Hakika kufanya hivyo ni hiana na makosa makubwa.

 

Mapambano Dhidi ya Ujinga na Upotevu

 

Ili kupambana na hali  hii mbaya yenye kusikitisha unaoishi umma wetu wa Kiislamu, panahitajika sana kuwepo moyo wa kimapinduzi na moyo wa kutaka kuleta mabadiliko na kuwa na msimamo wa kukataa na kupinga utaghuti (udhalimu).

 

Serikali za kidikteta na za kidhalimu zina­endelea kuzitwisha tawala zao kwa mataifa yetu manyonge na zinayatawala kwa siasa yao ya kikoloni na kwa kutumia njama za mataifa makubwa. Vilevile fikra za zamani zilizoyaweka nyuma mataifa bado zingalimo ndani mwa akili za viongozi wetu na wakuu wetu wa kidini na kijamii, na wakiwa katika wao wako katika hali kama hi wanauongoza umma wetu.

 

Nazo ada mbaya pamoja na mienendo iliyo chakaa ingali inazidi kuleta matatizo na vikwazo katika umma wetu. Kubakia nyuma katika maendeleo kunazidi, na udikteta unaotawala umetia fora. Haya ndiyo maisha tunayoishi kila siku na ndiyo hali iliyoenea katika umma wetu. Sasa imebakia tujiulize: Ni nini msimamo wa umma wetu juu ya kuishi katika hali kama hii na maisha kama haya? Hali ambayo inachoma mioyo yetu na kutuudhi?

 

Hakika ile roho ya kimapinduzi ya kutaka mabadiliko  na kukataa  kudhalilishwa iliyo­kuwemo ndani mwa nafsi za umma wetu ime­yeyuka kabisa. Msimamo wa kupinga ufisadi pia umetoweka. Nafsi zilizothubutu kupinga zime­kosekana. Mioyo yenye ghera na kaa lenye kuwasha utambi wa upinzani limezimika.

 

Kila mmoja wetu amekuwa akipuuza kila jambo isipokuwa yale mambo yanayohusiana na maisha yake tu. Hafikiri kitu isipokuwa mambo yanayohusiana na maslahi yake ya kibinafsi. Ama kufikiria hali ya umma au hali ya muundo wake wa kisiasa na kiuchumi, hayo yote ni mambo ambayo fikra yake haimpi nafasi kuya fikiria,  wala  hamu  yake haiyapi umuhimu wowote.

 

Hadi hivi sasa tungali tumebakia twaishi katika hali hi ya kupooza na kukosa thamani. Yawezekana watu wabadilike na mambo pia kubadilika na yakawa mengine, lakini hali yetu itabakia kuwa ni ileile ya ujinga, upotevu, kubakia nyuma katika elimu na uchumi na kutengwa kwenye uongozi wa nchi yetu. Tuta­bakia katika hali ileile ya kupomoka na kuwa katika dhiki na mateso. Tutabakia katika maisha haya na hali hii hadi pale roho ya kutaka mapin­duzi na mabadiliko itakapozaliwa upya ndani mwa nafsi zetu na mioyo yetu, na pale hisia za upinzani zitakapojumuika kwa wingi na tushu­ghulike na misimamo ya kupinga na kukataa hii hali yetu ya kubakia nyuma katika maendeleo yanayoenea.

 

Mwenyezi Mungu Mtukufu asema: "Hakika Mwenyezi Mungu hoyabadili yale yalioko kwo kaumu (watu) hadi (wao) wabadili yale yaliyomo nafsini mwao." (13:11)

 

Ikiwa tunaitamani roho hii ya kimapinduzi na tunataka kumiliki mioyo yenye kukataa na kupinga, basi katika kipindi cha ubarobaro ziko mbegu zilizo hai kabisa, na iko hali ya kima­umbile kabisa inayokubaliana kutekeleza matakwa haya. Na huu ndio wakati unaotakikana kwenda mbio kuitafuta roho kama hii.

 

Na hii ni kutokana na sababu zifuatazo:

Kwanza: Kijana huhisi kuwa na nguvu nafsini na viungoni mwake baada ya kuwa alikuwa aki­ishi katika hali ya udhaifu alipokuwa mdogo. Kutokana na sababu hii hujiona ana jukumu Ia kupinga na kukataa.

 

Pili: Tukimzingatia kwa makini tutamkuta kwamba kijana huanza maisha yake yungali hajavaana nayo bado wala hana pupa nayo kama wanavyoyapupia watu wakubwa, bali inakuwa kinyume chake,  yeye hupendelea kujitosa kwenye ukinzani na kukabiliana na hatari. Haya ndiyo yanayostahiki kuigwa na nafsi inayotaka kumiliki roho ya kutaka mapinduzi na kukataa.

 

Tatu: Kijana hana fungamano na maisha haya ya dunia wala hajaonja ladha zake zenye kum­fanya aipondokee. Na hii ni kutokana na muda mfupi aliyoishi hapa duniani na kwa sababu ya kutokuwepo maslahi mengi yenye kumvuta zaidi kuyapenda maisha haya.

 

Ni tabia ya binadamu kwamba anapoishi katika hali maalum kwa muda mrefu na maslahi yake yakawa mengi katika hali kama hiyo, huwa inakuwa vigumu kwake kufikiria kuibadili hali kama hiyo au maisha kama hayo, bali mara nyingine hupatwa na babaiko pakiwepo matara­ jio ya kupatikana mabadiliko.

 

(Kwa mfano, Jean Jacques Rousseau alikuwa akiona hali kama hiyo kwa ufalme wa Kifaransa. Yasemekana alikuwa akisema kwamba alikuwa akipatwa na babaiko kutokana na kuisawiri Ufaransa ikijiendeleza bila ya kuwa na mfalme, juu ya kuwa alikuwa ni miongoni mwa wanafikra na wanafalsafa wakubwa waliowaita watu katika kuendeleza hali ya kisiasa wakati ule. Hii ni kwa sababu Rousseau alikulia katika chombo cha utawala wa kifalme na kuvuta hewa yake kwa muda wote wa maisha yake).

 

Vivi     hivi utaona kwamba kundi Ia vijana ndilo kundi ambalo linaelekea zaidi kuwa na roho ya kutaka mapinduzi na kuleta mabadiliko, na wao ndio watu ambao wako tayari kabisa kuleta upinzani na kukataa ufisadi na dhuluma.

 

Ushahidi mkubwa ni hizi hoja zifuatazo: Tume zote zilizotoka mbinguni, mapinduzi yote ya kijamii yaliyofanyika yamefaidika na vijana. Vijana walitegemewa kama viongozi wa kuleta mabadiliko na kuwa kama nguzo ya kuyaendeleza mapinduzi.

 

Ama katika jamii zetu za Kiislamu kuna kosa kubwa linalotendeka katika kuamiliana na vijana wetu wanaokulia. Badala ya wao kuzikuza na kuziogoza roho zao ya kutaka mapinduzi na mabadiliko waliyonayo,  vilevile badala  ya kuiongoza roho ya kupondokea kwao katika upinzani, kuupinga ujinga ulioenea na upotevu uliotawala, sisi hufanya kila juhudi kuiua roho hii ya kimapinduzi iliyomo ndani mwa nafsi za vijana wetu. Pia huziua hamasa zao zilizowaka moyoni mwao ambazo ziko tayari kupambana na hali kama hizi. Mara nyingine utaona tuna­shughulika zaidi katika kutafuta njia za kuwa­kinaisha na kuwafanya wasalimu amri na kutii hii miweko ya ufisadi na kukubali kufuata hii miongozo michafu kwa njia za kuwavunja mioyo na kuzirudisha nyuma azima walizonazo na kuwakatisha tamaa nafsini mwao. Wakati huu tunapotumia hila za kuwakinaisha mabarobaro, huwa tunatumia kila mbinu na kila njia hata ikiwa ni kwa kuyapotoa baadhi ya mafunzo ya Kiislamu ili tu tuwakinaishe vijana wetu wasiweze kupinga au kukataa lolote analoambiwa.

 

Miongoni mwa tashwishi za kuvunja moyo ni ile itikadi ya taqiya (ufichaji wa imani), eti taqiya ni wajibu wa kisheria inayomruhusu mtu amnyamazie au amnyenyekee dhalimu yeyote anayetawala umma kwa dhuluma na maonevu!!

 

Eti kupambana ni kuiingiza nafsi kwenye maangamivu, na kufanya huko ni haramu katika sheria yetu ya Kiislamu!!

 

Eti  kufanya mapinduzi  au  kuleta aina yoyote ya mabadiliko  kunahitaji fatwa ya mujtahidi (mufti) ambaye haoni kuwepo maslahi kwa dini kwa hivi sasa kutoa fatwa!!

 

Eti fursa ya kufanya mapinduzi imepita kitambo, na ni wajibu kwa waumini kwa hivi sasa kungojea kudhihiri kwa Imam Mahdi!!

 

Hebu tafakari kidogo. Je, haya mafundisho na fikra hizi zisizo nyofu na zenye kupinga mapinduzi zinakubaliwa na vijana wetu wote? Vijana wanaotaka kuleta mabadiliko, waliojaa hamasa, walio na matumaini ya kuasi udhalimu na walio na lengo Ia kuhakikisha kupatikana mapinduzi watakubali fikra hizo?

 

La hasha!! Umma wetu na watu wetu wana akili imara zilizo madhubuti ambazo hufikiria na kuyapima mambo yanayotolewa na fikra hizi na mafunzo haya. Ndiyo, yawezekana wapatikane baadhi ya vijana ambao watahadaika na kukubaliana na hali hii ya ufisadi. Kisha waji­ondoe kwenye mkondo wa kutaka mapinduzi ambapo utawakuta wengine wanaitafuta njia ya mapinduzi popote ilipo ili waiandame hadi wahakikishe kwamba lengo lao Ia kuleta mabadi­liko limepatikana.

 

Hii ndiyo fursa wanayoipatiliza makundi ya upinzani na ndiyo nafasi inayopatilizwa na watu wenye hila za kikoloni ili wawawinde vijana wetu kwa jina Ia kuleta mabadiliko na maendeleo chini ya wito wa kupinga na kukataa.

 

Wakati ambapo kijana anapoona njia mbili mbele yake: njia  inayomwamuru kutii  na kunyenyekea upotevu na utaghuti (udhalimu) (kama wanavyoiona baadhi ya wapingamaende­leo), na njia inayomshajiisha kufanya mapinduzi na kumtia moyo wa kuleta maendeleo na mabadiliko - ni dhahiri na ni kawaida kwamba vijana wengi watafuata njia ya pili, kwa sababu njia hiyo inakubaliana zaidi na tabia yao na maumbile yao ya kutaka mabadiliko. Vilevile njia hi inachukuana na maumbile yao ya kutaka mabadiliko na inaafikiana na maumbile ya mwanadamu ya kutokata tamaa na kuwa na moyo wa matumaini usiokuwa na kifani.

 

Kwa hakika, tukizingatia, tutaona kwamba dhati au umbile Ia Uislamu ni mapinduzi, lina­pinga kubakia nyuma na linakataa dhuluma na upotevu. Tamko Ia KiisIamu Ia Laa ilaaha illa-Ilah (Hapana mungu mwingine anayeabudiwa ila Allah tu) linamaanisha kuwakufuru na kuwa­kataa waungu wote wa udikteta na upotevu.

 

Mafunzo ya Kiislamu yamemfaradhia kila binadamu aliyeukubali Uislamu kupambana na dhuluma,  kukomesha  ufisadi  na  ubatilifu, kukataa ujeuri na upotovu, na kuukomesha kabisa.

 

Lau sisi twasimama kwa nia safi na kufun­disha Uislamu halisi kwa vijana wetu pamoja na kuyaejezea mafunzo yake ya kimapinduzi na misingi yake ya kuleta mabadiliko, basi vijana wetu wangekuwa walinganifu, wenye nia safi ya kuuhudumia Uislamu, na wangekuwa wana­mapinduzi  wenye  kupambana kwa ajili ya kuuhuisha Uislamu na kuujenga umma wenye imani na wenye kuiongoza dunia.

 

Barobaro na Kujitolea katika

Njia ya Mwenyezi Mungu

 

Njia ya Mwenyezi Mungu ni njia ya haki, uadilifu na uhuru. Kuitumikia njia ya Mwenyezi Mungu ni kushughulika katika kuitekeleza haki, kuiandama na kuhakikisha kwamba uadilifu uko juu na uhuru uko kwa wote.

 

Matukio ya tarekhe (historia) na mazingira ya maisha yametufundisha na kututhibitishia kwamba  haki, uadilifu na uhuru haviwezi kupatikana ila kwa njia ya kupambana na kuji­toa mhanga. Umma ule unaomiliki roho yakuji­tolea, kujitoa mhanga na njia ya mapambano na mapigano unastahiki kupata uadilifu na uhuru ili ufikie anga Ia kuvuta hewa iliyojaa haki na usawa.

 

Ama umma ulio bahili na mwoga, jazaa yake ni kutawaliwa na tawala za kibatili, kidikteta, na kidhalimu ambazo zakandamiza umma na kuutia utumwani.

 

Na wale wanaongojea uadilifu na uhuru usimame na kuenea kila pahali kwa kuomba dua misikitini, kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, kutamani au kutumaini tu bila ya kusimama na kuyahakikisha hayo kwa vitendo, hao ni juu yao kuzidi kungojea dhuluma, maonevu, madharau, vitisho, n.k.

 

Uadilifu ni njia ambayo haimkiniki kuifikia ila kwa kulendea; uhuru wenye thamani haum­kiniki kupata ila kwa kuilipia. Njia ya kupata haki na uadilifu ni mapambano tu. Thamani ya kupata uhuru ni kujitoa mhanga, kujitetea na kuinyakua haki hiyo kwa nguvu.

 

Mtume Mtukufu amesema: "Kheri yote iko upangani.  Hakuna kinachowanyorosha watu isipokuwa upanga, na upanga ndio vishikilio vya Pepo."

 

Naye Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib akiwatahadharisha wale wanaopenda kujiweka nyuma kuuacha mkondo wa kujitoa mhanga na kujitolea kusaidia na wanaojitenga na kuiacha njia ya mapambano na kujikomboa, alisema:

 

"Jihadi ni mlango miongoni mwa milango ya Peponi. Mwenyezi Mungu ameifungua kwa wale mawalli Wake mahususi. Ni nguo ya uchaji Mungu, deraya ya Mwenyezi Mungu iliyo na hifadhi, na ni Pepo Yake iliyoimarishwa na inayotegemewa. Mwenye kuiacha (jihadi) kwa ajili ya kuichukia, Mwenyezi Mungu atamvika nguo ya udhalilifu na balaa itamwenea, na atadhalilika kwa madogo na matwevu."

 

Vijana wa umma ndlo walio na uwezo zaidi wa kupambana na kujitoa mhanga. Umbile lao na tabia yao wanayokuwa nayo katika kipindi hiki cha ujana huwavuta zaidi na kuwapambia kujiingiza kwenye mambo ya hatari bila ya kuyajali maisha, kwa sababu za kinafsi tulizo­tangulia kuzielezea katika faslu zilizotangulia.

 

Kwa hivyo, ni juu yetu kuihifadhi hii tabia iliyoko kwa wingi nafsini mwa vijana wetu. Tujibidiishe kuwaongoza kwenye njia ya kuji­tolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, yaani katika njia ya kuhakikisha kuisimamisha haki, kuusima­misha uadilifu na kuulinda uhuru.

 

La sivyo, umbile hili laweza kuelekezwa katika upande uliopotoka, na wakati huo kuta­patikana vikundi vya vitisho na mapote yenye kuleta uharibifu na upotevu. Vipote hivyo vita­kuwa na tabia ya kuilingiza kwenye ufisadi bila ya kujali, au vijana wetu watalelewa na makundi mengine maovu yaliyo kinyume chetu na kuwa­fanya wawe ndizo kuni za kuidumisha mipango yao ya uadui, au madaraja yao ya kuwavusha na kuwafikisha kwenye matakwa yao ya kikoloni.

 

Mafunzo ya Kiislamu Yazinduayo

Ndiyo Yanayotakikana Zaidi

 

Fikra huzinduka na kuamka. Bongo hufun­guka na alama za kuuliza huanza kuambata fikrani mwa vijana chipukizi. Maswali mengi humjia akilini mwake. Mimi ni nani? Kwa nini nimekuja ulimwenguni? Ni nani aliyeniumba na kunipa uhai?  Ni mwisho gani unaonisubiri ambao  utakomesha maisha yangu? Ni nini msimamo wangu katika jamii ninayoishi nayo?

 

Maswali kama haya na makumi mfano wake huchoreka ndani mwa akili ya kijana chipukizi na hubakia katika hali hii yakitafuta majibu ya maswali hayo ambayo yatapoza na kukinaisha moyo wake. Hi ni kwa sababu kijana huishi katika hali ya upungufu wa fikra na ni punde tu ambapo bongo lake hufunguka na kuanza kuya­fikiria mambo haya kwa makini.

 

Hi ndiyo fursa inayopatilizwa na makundi yaliyopotoka, yanayoingilia wakati kama huu ili kusimamia uandalizi wa fikra ya kijana kwa miongozo iliyopotoka ambayo hutayarishwa kwa ustadi na kwa lengo Ia kutupiga sisi wenyewe. Makundi haya huijaza fikra ya kijana kwa kumpa jawabu zenye upotevu ambazo si za haki katika kuyajibu maswali yake yaliyomo akilini na mawazoni mwake. Kutokana na sababu kama hizi ndiyo utaona kwamba mafunzo ya viongozi wa kidini yanatilia mkazo na kututanabahisha juu ya hatari ya kipindi hiki cha ujana kwa upande huu.

 

Mafunzo hayo na riwaya hizo zinawa­kumbusha wazazi, viongozi na wanavyuoni wa jamii yetu umuhimu wa kufanya haraka kupati­liza kuwaelimisha watoto na vijana na kuijaza faragha ya kifikra kwa itikadi sahihi za Kiislamu na kwa mafunzo yake yaliyo salama.

 

Uislamu unazingatia kwamba kumwelimisha mtoto ni haki mojawapo miongoni mwa haki za mzazi kwa mwanawe. Baba wa mtoto akiacha kutoa haki hiyo, basi Mwenyezi Mungu atamhoji na kumwuliza, na ikiwa atapatikana na makosa basi Mwenyezi Mungu hatasita kumtesa siku hiyo ya Kiyama. Imam Ali bin Husayn Zaynul Abidiyn AS amesema: "Ama haki ya mwanao, ujue kwamba yeye atokana nawe, na Akhera atawekwa nawe pamoja na kheri na shari zake. Nawe utaulizwa juu ya yote uliyomfunza katika adabu nzuri na katika kumthibitishia (Uungu wa) Mola wake Mwenyezi na Mtukufu na kumsaidia katika kumtii Mwenyezi Mungu. Basi mfanyie mwanao matendo mazuri na jueni kwamba mtalipwa thawabu kwa kumfanyia vizuri na mtateswa kwa kumfanyia maovu."

 

Ali bin Abu Talib AS ameitaja hali ya faragha ambayo kijana anayekulia huishi nayo. Ameitaja kwa kuashiria kwamba ni miongoni mwa sababu zinazomwandaa kukubali fikra yoyote anayoelezwa. Akasema: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa), chochote kinachoingizwa (kinacho­pandwa) hukikubali."

 

Imam Ja'far Sadiq AS anasisitiza kuharakisha kuelimishwa vijana wanaokulia ili kuwafutisha fursa mirengo iliyopotoka na kuwakinga kutokana na misingi inayobomoa. Asema: "Wapatilizeni watoto wenu wadogo kwa kuwafunza (Qur'ani na Hadithi) kabla hamjatanguliwa na wapingamaendeleo." Wapingamaendeleo (marjaiyyah) ni kundi lililokuwa na fikra zilizopotoka katika jamii ya Kiislamu katika zama hizo.

 

Leo katika zama zetu hizi tunaposhuhudia jinsi mawimbi ya upotevu yanavyoleta uharibifu na yanavyouweka Uislamu mbali na wengi wa vijana na mabarobaro wetu, na jinsi yanavyo­wavuta na kuwakumba vijana wetu waliozama katika malezi ya Mashariki na Magharibi, huwa hatuna budi ili kufikiria kwa makini misingi ya matatizo hayo na chanzo chake ili tuweze kupambana na haya mawimbi  ya upotofu ambayo yanahatarisha kwa kiwango kikubwa hali ya usoni ya umma wetu na ujumbe wa Kiislamu.

 

Si sahihi wala si kweli kwamba yote haya waliyonayo vijana wetu yanasababishwa na ubaya na uovu ambao uko ndani mwa nafsi zao. Vivyo hivyo, haifai kuzikubali fikra zilizochakaa za hao viongozi wapingamaendeleo ambao wana­yafasiri haya yote yanayotokea na kutendeka kwamba hayana bud  yatokee. Wana dalili kwamba ni lazima ufisadi udhihiri katika bara na bahari na ujeuri na dhuluma uenee ulimwenguni kote. Vivyo hivyo, wanasema kwamba haimki­niki kuyazuia yale yaliyokadiriwa na yaliyo­jaaliwa na historia.

 

Kwa jumla, udhaifu wa vijana wetu wa kutopendelea dini na kutoshikamana na mafunzo yake na badala yake kushikamana na mafunzo maharibifu yaliyoingizwa kutoka nje, unato­kana na sababu maalum zinazotokana na hali yetu ya kubakia nyuma katika maendeleo ya kila aina.

 

Sisi tuna jukumu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya historia katika suala Ia kupotea umma wetu ujao. Kwa sababu sisi ndio chanzo cha kupotea kwao na kwenda kombo. Kutokana na hali ya kujibakiza kwetu nyuma, kuacha kuwaongoza na kutojali kuwaelimisha hadi kufikia kiwango sahihi kinachostahili na kinacho­takikana.

 

Uislamu Uliopotoshwa

 

Miongoni mwa misingi muhimu na sababu zilizowasababisha  vijana  wetu  kuyatoroka mafunzo ya dini yao ni hii hali ya Uislamu ulio­potoshwa katika umma wetu wa kila mahali.

 

Kijana anapofumbua macho yake na kuiona jamii yake jinsi iliyotanikatanika katika mila, desturi na tabia, ilivyorudi nyuma katika elimu na maendeleo kadha wa kadha, ilivyotawaliwa na ubinafsi na ukabaiIa na badala yake kuthamini utabaka na dhuluma, au atakapoiona jamii hiyo ikiwa na fikra finyu na huko hayo yote hutendwa kwa jina Ia Uislamu na katika vazi Ia kidini, basi huchukulia kwamba yule mtawala au kiongozi hutawala kwa jina Ia Uislamu. Vilevile hudhania kwamba kilichosababisha watu kubakia nyuma ni mfumo wa Kiislamu.

 

Kwa kawaida, zile fikra za wale viongozi wapingamaendeleo zilizoganda hushikilia nafasi ya fikra za wanavyuoni halisi wa Kiislamu. Zile fikra ambazo hazikushikamana na mafunzo halisi ya KiisIamu na zilizojaa mafunzo ya woga na kupokonya moyo wa ushujaa, ndizo ambazo zinatangulizwa mbele ya watu ili zionyeshwe kama mafunzo sahihi ya Kiislamu.

 

Maadamu Uislamu unaonyeshwa na kufun­dishwa kwa mabarobaro wetu kwa sura kama hii iIiyochushwa ambayo inaonyesha kwamba ndilo chimbuko halisi lililosababisha umma kubakia nyuma, basi utakuwaje msimamo wa hao vijana wetu kuihusu dini hii?

 

Hapana shaka kwamba watautoroka Uislamu huu na kuyakataa mafunzo yake, na badala yake watatafuta njia nyingine waifuate ili waweze kuleta mabadiliko ndani ya umma, mabadiliko ambayo watayatarajia kulendeleza jamii yao.

 

Maisha haya ya kubaki nyuma, kuishi kwa jina na vazi Ia Kiislamu na kushikilia fikra hizo za kutotaka kuleta mabadiliko ambayo yanatoa picha iliyochafuliwa ya maendeleo ya Kiislamu, ndiyo sababu muhimu iliyowafanya vijana hao wanaokulia kuacha kushikamana na dini yao ya Kiislamu.

 

Wanajua Nini katika Dini ya Kiislamu?

 

Kabla hatujatoa mawaidha ya kuwashambulia, kuwakufurisha na kuwafanya mafasiki vijana wetu, ni wajibu juu yetu kujiuliza wenyewe:

 

Je, tumejaribu kuueleza Uislamu na kuwafunza kisha wao wakaukataa?

 

Jawabu ni la. Aghlabu ya vijana hawajui chochote katika mafunzo ya mfumo na misingi ya Kiislamu.Taaluma zote zilizokuwa zikifunzwa katika jamii zetu za Kiislamu, hazikukeuka hukumu za shaka katika masiala ya hedhi, nifasi, n.k. ambayo ni miongoni mwa mafunzo ya kifiqihi na kiibada.

 

Ama kwa upande wa fikra, uchumi, siasa au elimujamii ya Kiislamu, mafunzo haya muhimu hayakupatikana ila kwa uchache. Vijana wetu hawakuweza kuyapata mafunzo namna hii kwa urahisi. Je, haya yote si kweli? Katika hali kama hii ambapo kumeenezwa kasumba ya kila aina ya kupotosha na propaganda zinazotangazwa na mashirika pamoja na makundi  mbalimbali potofu, tunataraji nini kwao?

 

Wengi wa vijana walioyaepuka mafunzo ya dini na kuacha kushikamana na sheria zake walifanya hivyo kutokana na kutoujua kwao Uislamu,  kutojua  umbile  lake  tukufu  na umuhimu wake. Nasi tujue kwamba Mwenyezi Mungu atatuuliza kuhusu huu upungufu tulio­ufanya wa kutowafunza vijana wetu Uislamu halisi na kuwapa misingi ya mafunzo yake bora.

 

Vipi Tuifundishe Dini?

 

Mfalme aliota ndoto iliyomfadhaisha sana. Akaamka akiwa na fadhaa na hali ya kuingiwa na hofu. Akamwita mfasiri ndoto na kumwelezea yote aliyoyaona ndotoni. Akasema: “Nimeona meno yangu yakidondoka moja baada ya jingine. Hebu niambie maana yake ni nini?"

 

Mfasiri ndoto akainamisha kichwa kwa muda mfupi huku akifikiria, kisha akainua kichwa chake na kusema kwamba aliyoyaona yatakuwa kweli, na maana yake ni kuwa watu wote wa familia yake (mfalme) watakufa katika wakati wa uhai wake.

 

Tafsiri hi kavu yenye kisirani na fali mbaya ilimkasirisha mfalme  na kumtia hofu. Kwa hivyo, akaamuru mtaalamu huyo auawe mara moja. Kisha akaamuru aletwe mfasiri ndoto mwingine; na akaletwa haraka mbele yake. Mfalme akamwelezea ndoto ileile; naye mfasiri ndoto akamjibu jawabu kama ile iliyotolewa na mfasiri ndoto wa kwanza, kwamba watu wa nyumbani kwake watakufa katika wakati wa uhai wake. Jawabu hii pia haikumridhisha, na akaamrisha tena auawe.

 

Wakamletea mfasiri ndoto wa tatu. Tena mfalme akamwelezea ile ndoto kwamba ameya­ona meno yake yaking'oka moja likifuatiwa na jingine. Mfasiri ndoto huyo akamsikiliza kwa makini kisha akainamisha kichwa kufikiri; na baada ya muda kupita katika kuwaza na kuzinga­tia, akasema: "Ikiwa yale uliyoyaona ni kweli, basi wewe utakuwa mtu mwenye umri mrefu zaidi katika familia yako, inshaallah."

 

Jawabu hii iliufanya moyo wa mfalme kukunjuka na uso wake ukaonyesha furaha na kuondokewa na dhiki kutokana na tafsiri hiyo nzuri. Hivyo, akaamuru mfasiri ndoto apewe zawadi yenye thamani.

 

Msomaji mtukufu hebu zingatia kisa hiki. Je, unaona tofauti yoyote katika maana baina ya tafsiri hizo mbili? Ukweli ni kwamba hapana hitilafu. Zote mbili zinathibitisha hakika moja tu, nayo ni kuwa mfalme atabakia baada ya kuwakosa (kufa) watu wake wote. Basi kwa nini msimamo wa mfalme ulitofautiana mbele ya wafasiri ndoto hadi akaamuru wale wawili wa awali wauawe, na wa mwisho apewe zawadi?

 

Ukizingatia utaona kwamba siri kubwa me­fichika katika nija iliyotumika kueleza, kwani hakika ni ileile moja haikubadilika, lakini mara ya kwanza ilielezwa kwa njia inayoleta kisirani na kutisha, na mara ya pili ilielezwa kwa njia iliyojaa bishara, fali njema na furaha.

 

Mbinu ya Kuelezea ni Muhimu Sana

 

Katika kisa hicho imetudhihirikia wazi umuhimu wa mbinu ya kulielezea jambo lolote lile na umuhimu  wake katika kuhadidisha msimamo wa watu kutokana na jambo lililoelezwa. Hata ikiwa jambo moja ni la kweli lakini ikawa  halikuelezwa  kwa mbinu nzuri, basi hakuna dhamana kwamba watu watalikubali jambo hilo. Vivyo hivyo, ikiwa jambo jingine ni la batili lakini kukatumika mbinu nzuri katika kulielezea, basi huenda watu wengi wakahadaika na kulifuata.

 

Hivi sasa tunashuhudia vile hali ya watu kuelekea katika dini na kule kupungua katika kushikamana nayo. Tutaweza vipi kuwavuta na kuwaelekeza kwenye dini yao na kuwaelimisha ujumbe wao mtakatifu?

 

Ninaitakidi kwamba ni dharura mno kufikiria njia na mbinu nzuri ya kulelezea dini kwa watu. Wabalighi (wanatablighi) wengi na wanavyuoni hawajafaulu katika kuchagua ile mbinu nzuri, na kutokana na sababu hi hawakuafikiwa kufaulu katika shughuli zao, bali mara nyingine matokeo yake huwa kinyume chake na mara nyingine hutokea kwa baadhi yao upinzani na chuki ambavyo husababisha kuitoroka dini.

 

Qur'ani Tukufu inatuzindua juu ya umuhimu wa jambo hili katika kulingania Uislamu. Inasisi­tiza juu ya kutumia mbinu nzuri katika tablighi. Inasema: "Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa lile ambalo ni zuri." (16:125)

 

Pia Qur'ani yatuzungumzia kuhusu maadili (akhlaki) ya Mtume Mtukufu na taathira yake katika kuwavuta watu katika dini. Inasema: "Na lau ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu wangetawanyikatawanyika pembezoni mwako."

(3:159)

 

Tablighi na Hali ya Kijamii

 

Katika zama hizi hupatikana kila aina ya sababu ya kupotoa. Vyombo vya habari huhadaa kiasi cha kuathiri sehemu ya maisha ya kila siku. Imani ya kidini ya vijana wetu wa sasa ime­tingishika vya kutosha kutokana na hila za wakoloni na hali yetu ya kubakia nyuma. Hayo yote ni kwa sababu ya kuvutika kwetu zaidi katika upande wa ulimwengu wa Magharibi na Mashariki ambao wanamiliki kila aina ya vyombo vya maendeleo, teknolojia na elimu pamoja na maongozi yao ya kuupiga vita Uislamu.

 

Katika zama kama hizi na katika hali kama hii ya ufisadi, ni njia ipi bora inayoweza kuwa­vuta zaidi watu katika dini? Njia ambayo inawa­fanya wajitambue na wayarudie mafunzo yao ya Kiislamu? Hapa yapo mambo mengi ambayo ni wajibu yapatikane katika taratibu za kuielezea dini kwa watu katika zama zetu hizi.

           

Urahisi na Ufunufu

 

Sifa muhimu inayojipambanua nayo zama zetu hizi ni kuongezeka kasi na kufanywa mambo haraka haraka. Masafa  ambayo binadamu alikuwa akiyakata kwa ngamia katika muda wa mwezi mzima sasa anayakata kwa ndege kwa muda wa saa moja akiwa amekaa juu ya kiti chenye raha na starehe. Kazi ambayo binadamu alikuwa akiitolea juhudi na kutaabika kwa masiku, sasa anaifanya kwa masaa machache na kwa njia ya urahisi kabisa. Yote haya yamem­fanya binadamu kupendelea zaidi kasi katika shughuli zake na hata katika kufikiri kwake. Hii ni kwa sababu amechokeshwa kufanya jambo lolote ambalo linahitaji atoe juhudi nyingi na kupoteza muda mrefu.

 

Vilevile, hata katika upande wa kifikra na kielimu, usahali na ufunufu vimethibiti kuwa ndio wito wa fikra na elimu katika zama za sasa. Elimu ya falsafa iliyofanywa kuwa ngumu zamani na kusomwa na watu maalum tu walio na viwango maalum vya elimu, sasa imekuwa ikisomwa na mabarobaro wanaokulia. Vijana wamekuwa wakiisoma na kuijadili na kufuata msimamo wake mwenyewe mbele ya elimu hii. Vilevile tata za kielimu ambazo zilikuwa ziki­tatiza katika nyanja tofauti tofauti za elimu leo zimepoteza haiba yake. Zimekuwa zikiandamana na viwango vyote kutokana na kurahisishwa na kufafanuliwa kunakofanywa na vyuo, magazeti, majarida, vitabu, vipindi vya televisheni, n.k.

 

Kwa hivyo, tunapotaka kuyaelezea mambo yetu ya Kiislamu katika zama zetu hizi za kasi, usahali na uwazi, bila ya kupatikana uzito wowote, yatakikana tujiepushe na nija ngumu zisizofahamika. Tuyaelezee mambo ya kidini, kifikra na kielimu kwa taratibu zilizo funufu na rahisi ili kijana anayekulia aweze kuyafahamu na kuyashika. Na aghlabu huu ndio utaratibu unao­tumiwa na Qur'ani na uliotumika na Mtume Muhammad SAW katika kulingania kwake na katika maongozi yake.

 

Kuna baadhi ya wanavyuoni wanaopendelea kutumia mbinu ngumu na kuonyesha ubingwa wao wa kielimu katika hotuba zao na mihadhara yao na hata katika vitabu pia kwa kutumia misamiati na istilahi ngumu za lugha na mantiki wakati wanapoelezea mambo ya dini na mafun­disho yake matukufu. Taratibu kama hizi ni vizuri kuzitumia kwa wasomi walioelimika barabara, watu ambao wako tayari kutoa juhudi kuyatumia mabongo yao katika kufikiri. Ama yule mtu wa kawaida na kijana anayekulia, hana haja ya kuzisoma sentensi ngumu za lugha zisizo­fahamika. Wao huwa wamekwishazoea lugha rahisi ya magazeti.

 

Huenda baadhi ya wanafikra na wanavyuoni wakapunguza juhudi zao za kuwaandikia watu wa kawaida ambao hawajapevuka kielimu, lakini ukweli ni kwamba wao wanasahau kwamba watu wa kawaida ndio wanaohitaji zaidi kuongozwa na ndio wepesi zaidi kupotea au kupotezwa. Ama kwa upande mwingine, jambo lenyewe linahitaji kuwa na uwezo fulani wa kifasihi iIi kuzirahisisha fikra hadi zifahamike. Hii ni kazi ya mwanafikra au mwandishi kuifafanua fikra zake na kwa njia rahisi ili zifahamike mbele ya watu wa kawaida.  Haitokuwa  fahari kwa mwandishi  kuyaelezea  maandishi  yake kwa mbinu maalum iliyo ngumu, bali atashukuriwa na kusifiwa sana ikiwa atazielezea fikra zake kwa mbinu nzuri yenye kufahamika kwa urahisi.

 

Njia Zenye Kuathiri

 

Kuzieleza fikra fulani kwa njia isiyoeleweka huenda kukasababisha kutoziathiri nafsi au kuzifanya zile fikra zisivame au zisieleweke. Lau zatumika njia zilizo hai na zenye kusisimua njia hizi huzipa fikra hizo hisia zenye kuleta athari. Kwa mfano, kisa kizuri ambacho kime­kusudiwa kuielezea hakika fulani miongoni mwa hakika za kidini, chaweza kukubaliana na nafsi

na kuleta taathira zaidi kuliko vile yanavyoweza maneno ya kawaida kuathiri.

 

Watu wengine wamefaidika kiwango kikubwa kwa kutumia mtindo huu wa visa, wamezijaza maktaba zao kwa sampuli kadha wa kadha za visa vilivyojaa fikra zao na mafunzo yao. Nayo Qur'ani Tukufu imetangulia katika kutumia mbinu kama hizi. Utaona inaelezea vipande vingi vyenye kuathiri katika visa vya historia, nayo ina haki kabisa kuwa ndiyo visa vizuri zaidi. Hakika zilizotumiwa na elimu za kisasa za lugha za kuweka nambari na kudhibiti hesabu ni njia muhimu miongoni mwa njia za kuathiri katika zama hizi. Kwa hivyo, ni juu ya wabalighi wanao­ongoza kujisaidia kwa kutumia njia kama hizi katika kufundisha hakika za kidini. Vilevile wazitumie njia hizi katika kutolea ushahidi wenye kuyathibitisha mafunzo haya ya kidini na hukumu zake.

 

Kwa upande mwingine, ni wajibu juu yetu tusiuache uwanja wa fani chini ya maongozi ya wakoloni ambao ni msingi wa ufisadi na upotevu, kama vile, sinema, sarakasi na sanaa. Vyote hivyo ni vitu vyenye taathira kubwa katika nafsi ya mwanadamu. Lakini pamoja na masikitiko makubwa, vyote hivyo viko chini ya utumishi na utawala wa wafisadi na wapotofu. Ni juu ya wabashiri, wabalighi na wanavyuoni kujitahidi katika kufaidika na vitu mfano wa hivi ili kuya­tumikia malengo ya Kiislamu na mafunzo yake matukufu.

 

Umma Wenye Lengo

 

Binadamu wa sasa huishi katika hali ya kuji­amini kusiko na kipimo. Hutaka akifanye kila kitu kimnyenyekee ili ayashuhudie majaribio yake. Hatosheki na maelezo ya mhandisi juu ya umbo Ia nyumba au sampuli yake. Hata maelezo yake pia hayamkinaishi, bali mwishowe humtaka mhandisi amchoree ramani ya nyumba yenyewe ili aione kwa macho.

 

Akitaka kununua gari au chombo chochote kingine, mwanzo hutafuta maelezo yake ili akione kwa macho yake ndipo atoe msimamo wake. Binadamu hutumia njia hizi hata katika mambo ya kijamii. Kumwelezea uzuri wa nadharia fulani au ubaya wake hakumtoshelezi, bali hutaka aione nadharia yenyewe imechorwa na kutandikwa mbele ya uwanja wa kijamii ili aweze kuubaini msimamo wake juu ya nadharia hiyo. Ikiwa ataelezea juu ya nadharia fulani kisha baadaye ashuhudie kuwa watu wenye nadharia hiyo wanaishi katika hali iliyo kinyume chake, hatoweza kuamini kuwa fikra hii ni sahihi au ni sawa.

 

Kutokana na mantiki hii imekuwa ni dharura kupatikana jamii yenye imani ya msingi ili iwe ni dalili bora na ushahidi thabiti juu ya uzuri wa imani hii. Ni wajibu juu ya wanavyuoni, viongozi na wabalighi wawe ndio mbegu za kwanza kabisa katika kukuza hiyo jamii inayotakikana. Wayashike maadili ya Kiislamu na adabu zake katika muamala, maingiliano, maendeleo na maisha yao ili wayafanye kuwa ni kielelezo na kiigizo chema cha misingi ya dini na mafundisho yake.

 

Ama ikiwa sifa hizo hazitopatikana katika maisha ya wabalighi na wanavyuoni wa kidini, maneno yao na vitendo vyao vitakinzana na kupingana, na kitendo hiki kitatosha kuwa­kimbiza watu katika dini na kujiepusha nayo.

 

Mabarobaro na Uongozi

 

Wakoloni wanajaribu kutumia kila njia ya kimatendo katika kutawanya habari na kuwa­dhihirishia vijana wetu viongozi waliopotoka ili wawatumie vibaraka hao katika kuzielekeza hima za vijana wetu kwenye mambo ya kijinga na upotofu. Kwa ajili kama hii ndio tunaona wanatilia mkazo sana kuiongeza idadi ya viongozi wataalam, mabingwa wa riadha na makocha wa kijinsia. Lengo lao ni kuwapotosha vijana wetu na kuwafanya wawafuate na wawaige viongozi hao na waandame tabia na mienendo yao miovu.

 

Vilevile matangazo hayo ya kikoloni yanapo­taka kuwaelezea vijana wetu maisha ya shujaa fulani mwanamapinduzi na mtetezi wa haki, au yanapotaka kuelezea msimamo wa kijana shujaa au sira ya mwanafikra fulani, hujaribu sana kutoa habari za viongozi hao kinyume cha ukweli. Hutumia hiana, hila na huipotosha kabisa hakika ya viongozi hao au mashujaa hao na huwaarifisha kwa njia ambayo haitoleta faida yoyote kwa yule ambaye anaelezewa historia hiyo.

 

Ingawa sisi tunaheshimu kila taaluma na tunayatukuza mapambano yoyote ya kibina­damu, lakini wakati huohuo tunakataa kutenga­nishwa na historia yetu tukufu ambayo ni urithi wetu  mkuu uliojaa matukio matukufu ya mashujaa, wapiganaji jihadi na misimamo ya watetezi wa haki waliokuwa na ikhlasi. Urithi huo umejaa historia ya wanavyuoni wenye hima, nishati na uvumbuzi. Tunakataa kujisahaulisha historia za viongozi na mashujaa wa umma wetu watukufu na badala yake kuwaiga viongozi wa umma mwingine. Tunakataa kuwaingiza viongozi wengine hapa kwetu na kuwafanya kama viongozi kwa vijana wetu. Hii inamaanisha kuing'oa hadhi ya umma wetu na asili yake na kukata uhusiano baina ya vizazi vya sasa vya umma wetu na vile vilivyotangulia.

 

Tukizingatia tena tutaona kwamba mashujaa wa umma mwingine, viongozi wao, huenda msimamo wao na maongozi yao hayakuanza pale  panapochimbuka misingi yetu ya asili tunayoiamini. Vilevile harakati zao hazikulin­gana na yale maoni tunayoona na kuyaandama, wala hawalazimiani na yale mafunzo ambayo sisi tunalazimiana nayo. Ikiwa viongozi kama hao watakuwa ndio viongozi wa vijana wetu, basi kuna hatari ya kudanganyika na kushawishika.

 

Tunapoitupia jicho historia yetu tukufu tunaona kwamba vijana wetu waliobalighisha (waliosambaza) dini wana kipindi kikubwa cha kimsingi cha kuzingatiwa katika kuzitilia nguvu nguzo za ujumbe wa Kiislamu na kuujenga umma wa Kiislamu wenye imani na kutetea haki. Vijana wa Kiislamu ndio waliosimama msitari wa mbele katika kuyasimamisha mapinduzi ya Kiislamu, kuuendeleza mbele harakati zake na kuyalinda mafunzo yake.

 

Vilevile vijana wetu walikuwa katika kikundi cha mbele katika kuamini na kufuata upesi huu ujumbe uliotoka mbinguni hadi Mtume Mtukufu akasema:  "Ninawausia  (mwafanyie)  wema mabarobaro, kwani nyoyo zao ni laini zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amenituma nikiwa ni mbashiri na mhofishaji na mabarobaro wakani­unga na wazee wakanihalifu."

 

Kutokana na juhudi zao safi zenye ikhlasi, kujitolea kwao kukubwa na kumwaga kwao damu zao takatifu zilizo tohara ndiko kuliko­ufanya mti wa Kiislamu kutanda kijani kibichi na matunda yake yakaiva.

 

Sasa hebu tutoe baadhi ya harakati za vijana waliobalighisha dini iIi waigwe na vijana wetu wa Kiislamu wa leo kama viongozi wao.

 

Kuleta Mabadiliko katika Umma kwa Njia ya Hekima

 

Ikiwa tumekadiriwa kuzaliwa katika jamii hii iliyobakia nyuma, iliyoteseka na kuzidi kuji­bakisha nyuma, je, imeandikwa pia kwamba ni lazima tuishi maisha yetu yote tukiwa tunatawa­liwa na hali hii pamoja na mazingara haya? Ni kwa nini hatusimami kuibadili hali hii ili maisha yetu yawe na thamani na kuweko kwetu kuba­kishe athari?

 

Hakika wale wakuu ambao wanasifika katika historia na kuheshimiwa na kila umma walikataa kuyaacha maisha yakiwa yanaendelea kuishi katika hali ile waliyoikuta wakati walipokuja duniani. Wao ndio waliofanya bidii kuubadili umma wao, hali na mazingira yake, na ndio wale ambao kwamba wameitengeza historia na kuzi­chora athari zake. Majina yao yakabakia milele na majukumu yao waliyotenda na utukufu wao unashuhudiwa. Ama wale watu waliokuja katika jamii na kuondoka bila ya kuacha athari au sifa yoyote kama walivyokuwa, hao ndio wanafanana na wanyama, bali baadhi yao wamepotea njia zaidi, yaani hawana majina yatakayokumbukwa wala athari yenye kubakia.

 

Hapa upo mfano mzuri wa Mus’ab bin Umair, kijana aliyeishi katika raha, aliyependwa sana na wazazi wake na alikuwa mtoto wao wa pekee. Alikuwa na uwezo wa kufaidika na nafasi hii katika kuyajenga maslahi yake ya kibinafsi na kuijenga hali ya maisha yake ya baadaye, lakini alikataa kuishi kama mnyama mwenye hamu ya chakula tu. Hivyo, akajishughulisha na shughuli za kuleta mabadiliko na mapinduzi katika ile jamii ya Ujahilia na akavitumia vipawa vyake katika njia ya kuijenga jamii iliyokufa kiimani.

 

Mus'ab akajiunga na harakati za Kiislamu zilizokuwa zikiendeshwa kwa siri na hadhari katika mji wa Makka chini ya uongozi wa Mtume Mtukufu.

 

Kutokana na kujifunga kwake masombo na kushikamana na Uislamu, ameweza kutekeleza kwa bidii wajibu wake wa uongozi katika hara­kati za ujumbe wa Kiislamu. Na kwa ajili ya juhudi zake hizo, Mtume Mtukufu alimchagua kuwa balozi wake na mwakilishi wake katika Madina mji ambao baadae ukawa ndio kitovu cha Uislamu na matokeo ya jamii ya Kiislamu.

 

Mus'ab alifika Madina akiwa hamiliki silaha yoyote isipokuwa silaha ya ikhlasi na imani pamoja na malengo yake matakatifu ya kuleta mabadiliko na kupambana na maovu yaliyoenea.

Kulikuwepo ugomvi na tofauti za kijamii kati ya makabila ya Madina na hasa baina ya makabila mawili ya Aws na Khazraj. Kulikuwepo pia makundi ya kidini yaliyokuwa yakipingana

- Mayahudi, Wakristo na waabudu masanamu (washirikina). Vilevile ufisadi mwingi ulienea miongoni mwa vijana wa Ujahilia katika ulevi, kamari na upotevu mwingineo. Lakini Mus’ab yule kijana aliyekuwa akibeba wajibu wa ujumbe huu mtukufu, hakuwa na jingine ha kutekeleza wajibu wake katika kuleta mabadiliko katika jamii hiyo hata pangekuwepo vikwazo na matatizo ya aina gani.

 

Akaanzisha shughuli yake kwa mpango wake wenye hekima kupitia maongozi ya kiongozi wa ujumbe, na akaendelea na shughuli yake kwa ikhlasi na ustawi. Akapambana na matatizo kwa moyo mkunjufu, ushujaa na imani.

 

Haukupita muda katika Madina, harakati za ujumbe zilianza kupata vijana wakakamavu pamoja na umma ulioamini barabara malengo ya ujumbe. Mji wa Madina ukaanza kujiandaa kumpokea na kumlaki kiongozi wa ujumbe huu wa Kiislamu ambaye baada ya kufika tu aka­tangaza kuasisiwa kwa dola kuu ya Kiislamu.

 

Vivi hivi ndivyo Mus'ab alivyoweza kuibadili jami ya Madina - kutoka jamii uliyobakia nyuma hadi kwenye jamii yenye imani na iliyo hai ambayo ilisimama kupasua njia na kuieneza nuru na ujumbe wa Kiislamu.

 

Aliuhusisha Ubarobaro Wake Kuutumikia Uislamu

 

Watawala walio vibaraka wa wakoloni wana­endelea katika mbinu za kuwapoteza vijana wetu na kuuharibu ujana wao ambao ni kipindi kilicho na thamani zaidi maishani mwao. Kwa upande wa masomo, wanawapotezea wakati wao kwa kuwawekea vipindi na matangazo ya televisheni yenye  kuwapotosha na mambo mengineyo yenye kujaza bongo zao kasumba.

 

Kwa upande mwingine, binadamu hushangaa kutokana na hivi viwango vikubwa vya pesa vinavyozidi, pesa ambazo hutolewa na serikali katika uwanja wa michezo na starehe kutokana na uchumi wa wananchi. Je, yote haya ni kuto­kana na kwamba eti serikali hizi zinataka kuwa­punguzia wananchi wake baadhi ya shida zao au zinataka kuwastarehesha?

 

La hasha! Lau ni kweli kwamba serikali hizo zinawatakia raha wananchi wake, zingewajengea viwanda vidogovidogo vya kazi za mikono au kuwafanyia miradi inayohitajika katika maisha yao. Wananchi wengi wanashtakia upungufu wa huduma za siha, afya na mahitaji muhimu ya kijamii. Hakuna majumba ya kukaa wala misaada ya kimaisha. Badili ya kusaidia upande huu muhimu, serikali hutoa misaada kwa ajili ya riadha kwa kadiri kubwa. Kwa nini?

 

Jawabu liko wazi kabisa. Inataka kuipitisha bure fursa ya kijana kwa wananchi ili umma wetu usifaidike naye katika kuujenga mustakbali wake.

 

Inataka kuzishughulisha nyakati za vijana wetu na kuzipondoa hamu zao ili wasipate wakati wa kufikiria haji wanayoishi watu wao wala wasifikirie kupanga jinsi ya kuwaokoa.

 

Inataka kuviyeyusha vipawa na ujuzi wa vijana wetu ili daima tubaki kuwa ni mateka wa vipawa vya wataalam wa kigeni.

 

Inasikitisha sana kuona kwamba vijana wetu wengi wameingia kwenye mtego huo mbaya na lengo hilo bovu lililojaa hila za wakoloni na mabeberu. Vijana wetu  wengi  wanapoteza nyakati zao za thamani na umri wao mtukufu katika riadha na michezo mingine ya upuuzi. Kwa mfano, hujitahidi kujinyakulia ubingwa katika kucheza mpira wa miguu, ha mara nyingine huishi katika hali ya mapambano katika nyanja na vilabu vya riadha badala ya kushika­mana na mapambano ya kiasili ambayo ni wajibu juu yake kujiingiza kwa ajili ya kuyatetea maslahi ya umma wake na ujumbe wake.

 

Je, wakati haujafika bado kwa vijana wetu kutambua upeo wa njama hizi ili wayaache michezo ya upuuzi na wazielekeze hima zao na vipawa vyao katika mambo yaliyo wajibu maishani mwao?

 

Ni  viongozi  wangapi waliotajwa katika historia yetu tukufu ambao walishughulikia kipindi cha ujana wao kwa ajili ya kuuhudumia Uislamu na kuujenga mustakbali wa jamii zao?

 

Hebu tumwone Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib AS. Akiwa mdogo bado aliiweka nafsi yake kuutumikia ujumbe wa KiisIamu. Alikuwa ni kijana wa kwanza kusilimu na kusadiki Utume wa Mtume Muhammad SAW pamoja na kwamba umri wake haukuzidi miaka tisa. Wakati watoto wa Makka walipokuwa wakiongozwa na mafasiki kumwudhi Mtume Mtukufu na kumtupia mawe alipokuwa akitembea barabarani, Ali alikuwa kijana wa miaka kumi akiandamana na Mtume Mtukufu njiani akimwondoshea udhia na kuwa­adhibu watoto hao wa makafiri.

 

Vilevile katika usiku wa Hijra, kijana 'Ali alionyesha upeo wa kujitolea kwake na imani yake thabiti. Washirikina waliizingira nyumba ya Mtume Mtukufu wakitaka kumshambulia na kumwua Mtume Mtukufu wakati wa alfajiri. Ikawa hapana budi ila Mtume Mtukufu atoke kwa muda mle nyumbani ili aweze kuanza safari yake ya Hijra. Mtume Mtukufu akamtaka Ali -nduguye, na binamu yake ambaye wakati huo alikuwa ni kijana mbichi kabisa, achukue nafasi ya kuwahadaa maadui kwa kulala katika kitanda cha Mtume Mtukufu hadi asubuhi wakati watakaposhambulia maadui. Pamoja na kwamba kulikuwepo hatari kubwa katika kuliingilia jambo kama hili, lakini hata hivyo alilala juu ya kitanda cha Mtume Mtukufu huku akingojea panga na mikuki ya maadui kwa moyo thabiti na ushujaa kamili.

 

Baada ya Mtume Mtukufu kuhajiri Madina, Ali alikuwa ndiye mwakilishi wake katika Makka. Amana alizokabidhiwa Mtume Mtukufu akazi­rudisha kwa wenyewe. Akasimamia harakati za Kiislamu na kuihami familia ya Mtume Mtukufu. Kisha naye akagura pamoja na familia ya Mtume Mtukufu hadi Madina ingawa kwamba kuli­kuweko na upinzani mkubwa pamoja na kufu­kuzwa na washirikina njiani.

 

Mjini Madina alikuwa pamoja na Mtume Mtukufu katika shughuli na harakati zake zote. Kutokana na ushujaa wake, Mwenyezi Mungu aliunusuru Uislamu na kuupa ushindi katika vita vyote alivyoshiriki.

 

Kijana Ali aliuhusisha ujana wake katika kuuhudumia ujumbe wa Kiislamu hadi akawa mzee na akauawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

 

Karibu na ushahidi wake alisema: "Hakika nimeanza nao (Uislamu) na mimi nilikuwa chini ya miaka ishirini, na hivi sasa nimezidi miaka sitini.”

 

Barobaro Mwanamapinduzi Shahidi

 

Alikuwa ni kijana chipukizi mwenye umri wa miaka kumi na nane. Alikuwa na uzuri wa ajabu, tabia njema na mwerevu. Alifanana sana na Mtume Mtukufu kwa tabia na umbo kama alivyosema baba yake Imam Husayn bin Ali AS. Huyo ni Ali Akbar, mwana wa lmam Husayn AS.

 

Kijana huyo mtukufu aliandamana na baba yake Husayn katika harakati zake dhidi ya dhuluma na upotevu wa Bani Umayya. Kuanda­mana kwake pamoja na baba yake hakukutokana na huruma itokanayo na fungamano Ia nasaba, bali kulitokana na imani yenye kanaa na lengo, na nia yenye chimbuko Ia kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu.

 

Wanahistoria wanaelezea kuwa katikati ya njia walipokuwa wakielekea kwenye medani ya vita na mapambano, kiongozi wa mapinduzi, Imam Husayn AS alisinzia kidogo na alipotana­bahi akawa analikariri neno: "Inna Lillaahi Wainna llayhi raaji’unna." (Sisi ni wa Mwenyezi Mungu nasisi tutarudi Kwake).

 

Mwanawe Ali Akbar alikuwa ubavuni karibu naye, akamwuliza: "Baba! Kwa nini ulilikariri maneno hayo? Mwenyezi Mungu asikuonyeshe baya." Imam Husayn AS akamjibu: "Ewe mwa­nangu! Nimefazaika. Nimemwona mtu aliye­panda farasi akisema: 'Watu hawa wanakwenda na mauti yanawaandama.'” Ali Akbar akasema: "Ewe baba! Kwani sisi hatuko kwenye haki?" Baba yake akamjibu haraka: "Kwa nini! Wallahi sisi tuko kwenye haki!" Ali Akbar akasema: "Basi wallahi hatutojali tuyaangukie mauti au mauti yatuangukie."

 

Msomaji tazama! Mambo hayo kwake haya mhusu baba yake bali yanahusiana na haki na kwa ajili ya haki. Kwa hivyo, kustahamilia yaliyo machungu na kukabiliana na mauti huwa sahali kwa mtu.

 

Kwa hakika, askari wa upande wa maadui walijaribu wawezavyo kumvuta Ali Akbar ili ajiunge nao au kwa uchache wamtenganishe na askari wa baba yake kwa kupatiliza uhusiano wa nasaba kati ya Ali Akbar na Yazid bin Muawiya yule mpotevu aliyejibandika kuuongoza umma wa Kiislamu kwa ubatilifu. Mama wa Ali Akbar ni Layla bint Abu Murrah bin Urwa bin Masud al-Thaqafi. Mama yake ni Maymuna bint Abu Sufyan, dada yake Habiba, mke wa Mtume Mtukufu. Kwa hivyo, nyanya wa Ali Akbar ni dada wa Muawiya na ni shangazi wa Yazid.

Baadhi ya makamanda wa jeshi Ia lbn Saad walimwita katikati ya vita wakati ilipobainika wazi kwamba mwisho wa watu wa Imam Husayn AS na Ahlul Bait yake ni kifo na ushahidi. Walimwambia Ali Akbar: “Wewe ni jamaa wa Amirul Mu'miniyn Yazid, na wala hatupendelei ufikwe na ubaya wowote. Njoo kwetu."

 

Lakini Ali Akbar kijana mwanamapinduzi, hakuwa mtu mwenye kuhadaika au kukubali huu wito mwovu wenye hiana. Akawajibu papo hapo: "Upotevu ni wenu. Ujamaa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi uchungwe kuliko uakraba wa mwana wa mla maini."

 

Akawakumbusha kuwa heshima zao za ubatilifu walizoshikana nazo ni duni kuliko zile alizoshikana nazo yeye - heshima za haki na uongofu. Wao walikuwa wanautukuza utawala wa kidhalimu na kuheshimu zaidi fungamano lao na utawala huo huku wakidharau na kutupa kando fungamano na heshima kwa Mtume Mtu­kufu na kuhifadhl haki ya kuunga uzao wake. Kisha akaingia medani katika vita vya jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Akadhihirisha ushujaa mkubwa na kuwashangaza maadui ambao wali­lazimika kumchagua yule shujaa wao zaidi kwenda kupambana naye. Mwishowe kijana huyu mtukufu akaanguka ardhini akiwa ame­kufa shahidi juu ya ardhi ya ushahidi ili aandike kwa damu yake wasia kwa vijana wa umma wa Kiislamu utakao kuja karne za baadae, kwamba wasimame kutekeleza wajibu wao katika kuu­tetea ujumbe wa Kiislamu na kuzitetea haki na maslahi ya umma. Vijana wanaharakati watafute ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wasi­ogope wala wasijali kuyaendea mauti au kufikiwa na mauti.

 

Hadithi Kuwahusu Mabarobaro

 

Zifuatazo ni hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume Mtukufu  SAW  na Maimamu Maasumu AS kuhusu vijana:

 

Vijana Wajielimishe

 

Imam Baqir AS:  "Lau namjia barobaro miongoni mwa mabarobaro ambao ni wafuasi wetu, nikamkuta hajifunzi katika dini, ningemwadhibu." (Safinatul Bihar, jz. 1, uk. 680)

 

Kujifunza Ujanani

Mtume Mtukufu SAW:  "Mwenye kujifunza katika ujana wake ni kama kuchora katika jiwe." (Usuulul Kaafi, jz. 2, uk. 603)

 

Qur'ani Huvaana na Kijana

 

Abu Abdillah AS: "Mwenye kusoma Qur 'ani akiwa ni kijana muumini, Qur'ani hutangamana na nyama yake na damu yake, na Mwenyezi Mungu Mtukufu humweka pamoja na watukufu na watiifu, na Qur'ani itakuwa ni kinga yake siku ya Kiyama." (k.j., jz. 2, uk. 603)

 

Upatilize Ujana Wako

 

Mtume Mtukufu SAW alimwusia Abu Dharr: "Ewe Abu Dharr! Yapatilize (mambo) matano kabla ya matano: Ubarobaro wako kabla ya uzee wako; siha (afya) yako kabla ya ugonjwa wako; utajiri wako kabla ya umasikini wako; faragha (nafasi) yako kabla ya shughuli zako; na uhai wako kabla ya kifo chako." (Abu Dharr Thairi 'Adaalatul lslaamiyyah, uk. 23)

 

Enyi Barobaro Itakeni Akhera

 

Salaam bin Miskiyn amesema: "Imam Hasan AS ametuambia: 'Enyi kundi la mabarobaro! jilazimisheni kuitafuta Akhera; hakika wallahi tumewaona watu waliotafuta Akhera wakapata dunia na akhera. Wallahi hatujaona mwenye kuitaka dunia akaipata Akhera.' " (al-Irshad; uk. 57)

 

Imam Mahdi Atakuja akiwa Barobaro

 

Abu Abdillah AS:  "Lau Qaim Imam Mahdi AS atasimama watu watamkataa kwa sababu atawajia akiwa ni kijana kabisa. Na miongoni mwa balaa ni kuwatokea watu huku akiwa ni barobaro na wao wakimtarajia kuwa ni mtu mzima." (al-Ghaybatul Kubraa, uk. 11)

 

Barobaro ni Mwepesi Kiyaendea ya Kheri

 

Abu Jaafar al-Ahwal alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa Imam Sadiq AS aliyekuwa akijishughulisha  kuyatangaza  mafunzo ya Kiislamu na Ahlul Bait. Siku moja Imam Sadiq AS alimwuliza: “Je, waionaje hali ya watu katika kulijia jambo hili (dini) na kuingia ndani yake?" Abu  Jaafar akasema:  "Wallahi!  Hakika ni wachache sana." Imam Sadiq AS akasema:

"Jilazimishe na vijana, kwani wao ni wepesi katika kuyaendea kila (mambo ya) kheri." Jawaan, uk. 49)

 

Upatilize Uvulana Wako

 

Imam Ali AS: “Upatilize uvulana wako kabla ya kuzeeka kwako, na afya yako kabla ya kuugua kwako." (k.j., uk. 60)

 

Enyi Vijana Fanyeni Bidii na Mjitahidi

 

Mtume Mtukufu SAW: "Mwenyezi Mungu anaye malaika ambaye huteremka kila usiku kutangaza: 'Enyi vijana wa miaka ishirini! Fanyeni bidii na mjitahidi.'  (k.j., uk. 66)

 

Faragha ya Kifikra kwa Barobaro

 

Imam Ali AS: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa) cho­chote, kinachoingizwa (kinachopandwa) ndani yake hukikubali." (k.j., uk. 69)

 

Jihifadhini kwa Elimu na Adabu

Imam Ali AS:  "Enyi kundi la vijana! Ihifa­dhini heshima yenu kwa kujifunza adabu ya dini yenu na kujielimisha." (k.j., uk. 194)

 

Barobaro Awe Mwalimu au Mwanafunzi

 

Imam Sadiq AS: "Sipendele kumwona kati yenu ila anakuwa katika hali mbili - Ama awe aalim (mwalimu/mwanachuoni) au mwanafunzi. Ikiwa hakufanya hivyo atakuwa amepoteza (amepunguza juhudi), na mwenye kupunguza juhudi hupoteza, na akipoteza hupata dhambi, na akipata dhambi huingia Motoni. Naapa kwa yule aliyemtuma Muhammad kwa haki." (k.j., uk. 197)

 

Barobaro Huisumbua Nafsi

 

Imam Ali AS: "Asiyeisumbua nafsi yake udogoni (kwa kujielimisha) hatokuwa mwerevu ukubwani.” (k.j., uk. 278)

 

Ni Nzuri Zaidi Wakati wa Ujana

 

Mtume Mtukufu SAW:  "Kutubu ni kuzuri, lakini kwa barobaro ni kuzuri zaidi." (k.j., uk. 297)

 

Nani Atambuaye Ubora wa Ubarobaro

 

Imam Ali AS: "Hajui ubora wa vitu viwili ila mwenye  kuvikosa - ubarobaro na afya." (Ghurarul Hikom wa Durarul Kalim, uk. 199)

 

Utaulizwa Kuhusu Ubarobaro Wako

 

Mtume Mtukufu SAW: "Hazitanyanyuka nyayo za mja juu ya sirati siku ya Kiyama hadi aulizwe kuhusu umri wake ameumaliza katika kitu gani na ubarobaro wake ameuchakaza katika nini?" (k.j., uk. 7)

 

Umeupoteza Wapi Ubarobaro Wako

 

Imam Sadiq AS: "Miongoni mwa mawaidha aliyotoa Luqmaan kumwambia mwanawe ni:

'Ewe mwanangu. Jua ya kwamba wewe kesho utakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu Aliye Mshindi na Mtukufu utaulizwa kuhusu mambo manne: Ubarobaro wako umekwisha katika nini?  Umri wako umeumaliza katika jambo gani? Mali yako umeichuma kutokana na nini? Na umeyatumia katika nini?'" (k.j., uk. 8)

 

Barobaro katika Kivuli cha Mwenyezi Mungu

 

Mtume Mtukufu SAW: "Watu saba Mwenyezi Mungu atawafunika katika kivuli Chake siku ambayo hakutakuwapo kivuli chochote isipo­kuwa Chake: Imam mwadilifu, barobaro aliye­kulia katika kumwabudu Mwenyezi Mungu..." (k.j., uk. 350)

 

Barobaro Mwenye Kutubu

 

Mtume Mtukufu SAW: "Hakuna kitu kinacho­pendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kuliko baro­baro mwenye kutubu." (k.j., uk. 350)

 

Kupatiliza Kuwaelimisha Vijana

 

Imam Ja'far Sadiq AS:  "Wapatilizeni vijana wenu kwa kuwafunza hadithi kabla hamjatangu­liwa na wapingamaendeleo." (k.j., uk. 352)

 

Wapingamaendeleo Huepukwa na Barobaro

 

Imam Ja'far Sadiq AS: "Enyi kundi Ia vijana! Mwogopeni Mwenyezi Mungu wala msiwaendee watawaIa (waovu) waacheni (waepukeni) hadi wawe mikia (wakose thamani) (k.j., uk. 66)

 

Mabarobaro Washikamana na Mtume Mtukufu

 

Mtume Mtukufu SAW:  "Nawausieni mwa­fanyieni wema vijana, kwani wana mioyo laini zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu amenituma mimi (niwe) mbashiri na mhofishaji. Vijana wakaapa kushikana nami na wazee wakanihalifu. . . Na muda wao (wa kuishi duniani) ukawa mrefu na nyoyo zao zikasusuwaa." (k.j., uk. 248)

 

Heshima Hupatikana kwa Elimu

 

Imam Ali AS: "Jifunzeni elimu mkiwa vijana mtatukuka kwayo mtakapokuva wakubwa.” (k.j., uk. 400)

 

Mkitaka Kuendelea

 

Imam Ali AS: "Asiyejifunza ujanani hata­endelea ukubwani." (k.j., uk. 400)

 

Vijana Wajifunze Nini?

 

Imam Ali AS: "Yaliyo bora kwa vijana kuji­funza ni yale mambo watakayoyahitajia wata­kapokuwa wakubwa." (k.j., uk. 401)

 

Onyo Juu ya Kupotoka Barobaro

 

Mtume Mtukufu SAW: "Mtakuwaje wata­kapoharibika wake zenu na vijana wenu kuwa mafasiki, na mkaacha kuamrisha mema na mkaacha kukataza maovu?" (Tuhaful 'Uquul, uk. 41)

 

Kutoa Miongozo kwa Vijana

 

Amirul Mu'miniyn AS amemwusia mwanawe Hasan AS hivi: “Hakika moyo wa kijana ni mfano wa ardhi ambayo haina kitu (mimea) na cho­chote kinachopandwa ndani yake hukikubali (hustawi). Kwa hivyo, nimekupatiliza kuku­funza adabu kabla moyo wako haujawa mwovu na kabla bongo lako halijashughulika, ili uweze kupokea kwa juhudi za rai yako lile jambo ambalo wamekutosheleza nalo kulitaka na kuli­jaribu wenye majaribio. Utakuwa umetoshelezwa taabu ya kutafuta na kuyajaribu majaribio. Yakakujia kutokana na hayo ambayo tulikuwa tukiyaendea na yakakubainikia kutokana na hayo ambayo huenda hayakutufungukia." (k.j., uk. 53)

 

Ubarobaro Huenda Ukawa ni Ulevi

 

Amirul Mu'miniyn AS:   "Ulevi ni wa aina nne: Ulevi wa ubarobaro, ulevi wa mali, ulevi wa usingizi, na ulevi wa ufalme." (k.j., uk. 88)

 

Hatari ya Kutekwa Vijana

 

Amirul Mu'miniyn AS: "Mara nyingine bina­damu wakati anapokuwa na nguvu (afya) na ubarobaro, hujiwa na hali ambazo huyapupia makosa. Kwa hiyo, mayowe na nguvu humshajiisha; moyo wa matamanio humpambia; moyo wa mwili humwongoza hadi ukamtia kwenye makosa (hayo) na akiyatenda makosa huepushwa kutokana na imani, na imani nayo humwepuka." (k.j., uk. 134)

 

TAMATI

 

SAW:    Sallallaahu alaiyhi wa-aali, m.y. baraka za Mwenyezi Mungu ziwe kwake na kwa aali (wazaa) wake.

AS:       alayhis/alayhas/alayhimus salaam, m.y. amani iwe juu yake/yao.

k.j.:   kama juu.


 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.